Header Ads Widget

WIZARA YA AFYA YATOA TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA MPOX NCHINI

 


WIZARA ya Afya mnamo tarehe 7 Machi, 2025 kupitia mifumo yake ya ukusanyaji wa taarifa na ufuatiliaji wa magonjwa ilipokea taarifa za uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Waziri wa Afya, Jenista J. Mhagama (Mb) imeleeza:

Dalili hizo ziliambatana na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo.

Kati ya wahisiwa hao mmoja ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam. 

Baada ya kupokea taarifa za wahisiwa, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Taifa kwa uchunguzi.

Mnamo tarehe 9 Machi, 2025 uchunguzi wa kimaabara umethibitisha kuwa wahisiwa wawili (2) wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox.

Hivyo, hadi kufikia sasa jumla ya wahisiwa wawili (2) wamethibitika kuwa na ugonjwa wa Mpox nchini.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na vituo vyote vya kutolea huduma za Afya, inaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna wahisiwa wengine ili waweze kupatiwa huduma stahiki. 

Chanzo cha ugonjwa huu ni wanyama jamii ya nyani, ambapo binadamu huweza kuupata 

kutokana na shughuli zinazoweza kusababisha kugusana na wanyama, majimaji au nyama za wanyama wenye maambukizi.

Aidha, endapo binadamu akipata maambukizi hayo anaweza kumwambukiza mtu mwingine kwa kugusana moja kwa moja. 

Kwa taarifa hii, Wizara ya Afya, inawahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga kudhibiti ugonjwa huu na hasa kutokana na uzoefu tulionao wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko. 

Serikali inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote, upimaji wa watu wanaoingia na kutoka kupitia mipaka ya nchi, kuimarisha utoaji wa elimu ya afya na kuhamasisha jamii ili kuwawezesha wananchi kuchuka hatua za kujikinga.

Kwa kuzingatia kuwa magonjwa mengi yanayosababishwa na virusi hayana tiba mahususi ila mgonjwa anahudumiwa kulingana na dalili alizonazo.

 Hivyo Wizara inawasihi na kuwasisitiza wananchi wote kuzingatia na kutekeleza afua za kujikinga kama ifuatavyo:

i. Kuwahi katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu unapoona 

mojawapo ya dalili za ugonjwa wa Mpox au piga simu nambari 199 bila malipo;

ii. Kuepuka kuchangia vitu kama nguo na matandiko ambavyo vimetumiwa na mtu mwenye dalili za Mpox;

iii. Kuepuka kugusana kwa kupeana mikono, kubusiana, kukumbatiana au kujamiiana na mtu mwenye dalili za Mpox;

iv. Kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za Mpox.

v. Kuepuka kumuhudumia mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox bila kuchukua taharadhari;

vi. Watumishi wa afya kuzingatia kanuni za kujikinga na magonjwa wakati wote 

wanapowahudumia wagonjwa ikiwemo wenye dalili za vipele na homa;

vii. Kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.

Wizara ya Afya, itaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa huu, kadri taarifa za

ufuatiliaji na uchunguzi zitakavyopatikana. Wizara inashauri wananchi kuendelea na shughuli za kila siku kwa tahadhari za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu.

Vilevile, Wizara inapenda kuwapa taarifa kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa 

Marburg, ikumbukwe kwamba, mnamo tarehe 20 Januari 2025, Serikali ilihabarisha 

umma hukusu kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg. Mwenendo wa 

udhibiti wa ugonjwa huu unaendelea vizuri na hadi kufikia leo tarehe 10 Machi 2025,

zimetimia siku 41 bila kuwa na mgonjwa mpya. 


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI