NA ARODIA PETER
MATUKIODAIMA App, MOROGORO
WAZIRI Mkuu, Kasim Majaliwa ameonya kuwapo uzembe katika kusimamia ulinzi wa mazingira, akisema kunachangia uharibifu wa vyanzo vya maji nchini.
Ili kukabiliana na hilo, Majaliwa ametoa maagizo saba kwa kuziagiza halmashauri zote nchini kuzingatia utunzaji wa mazingira na kuifanya iwe ni ajenda ya kudumu ikiwa ni pamoja na kutunza vyanzo vya maji.
Waziri Mkuu alitoa onyo hilo jana, Machi 5, 2025 baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa bwawa la maji Kidunda lililopo Tarafa ya Ngerengere mkoani Morogoro.
Alisema mradi huo mkubwa wa Kidunda ambao umegharimu Shilingi bil 335 fedha za nsdani hautokuwa na maana endapo vyanzo vyake vya maji havitatunzwa sawasawa.
Alisema mradi huo ni mojawapo ya mkakati wa kitaifa unaolenga kauli mbiu ya ‘kumtua mama ndoo kichwani’, hivyo wadau hususan wananchi, mamlaka za vijiji hazina budi kuhakikisha hakuna uharibifu wowote wa mazingira katika eneo lao.
“Tunayo migogoro mikubwa ya utunzaji wa mazingira na katika miaka ya 2021/2022 kulisababisha ukame wa kutisha. Sasa naziagiza halmashauri utunzaji wa mazingira iwe ni ajenda ya kudumu ikiwa ni pamoja na kutunza vyanzo vya maji.
“Naziagiza mamalaka zote za mikoa, wilaya kuainisha vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kuvitungia sheria ndogo sambamba na utoaji wa elimu ya mazingira.
“Aidha wakurugenzi wa mabonde acheni kukaa ofisini, tembeleeni mabonde yenu na maeneo yenye changamoto muyajue, vibali vya matumizi ya maji viwekewe utaratibu, shirikisheni sekta binafsi zinazofanya vizuri pamoja na wananchi.”alisema Majaliwa.
Akitoa taarifa ya mradi wa bwawa la Kidunda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema mkataba wa ujenzi wa bwawa hilo uliingiwa baina ya wizara yake kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) na mkandarasi Ms Sinohydro Corporation Ltd ya China.
Alisema mhandisi mshauri wa mradi huo ni Ms Ghods Niroo Engineering Company ya Iran kwa ubia wa Ms Advance Engineering Solution (T) limited ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi Bilioni 335, huku ujenzi huo ukiwa umefikia asilimia 28.
Waziri alisema, maji yatakayozalishwa kwenye bwawa la Kidunda yatasambazwa katika kata nne ambazo ni Ngerengere, Matuli, Mkulazi na Selembala za mkoani Morogoro, Dar es Salaam na Pwani.
Mwisho
0 Comments