Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodom
SERIKALI kupitia Bohari ya dawa (MSD) imesema itaendelea kuboresha huduma za dharura za uzazi
pingamizi na huduma za awali kwa watoto wachanga ambapo kwa kipindi cha miaka minne imenunua na kusambaza bidhaa za afya, kwa ajili ya kuboresha vituo vya afya 316 na kuhakikisha vinatoa huduma ya dharura ya uzazi na mtoto .
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai amebainisha hayo Jijini Dodoma kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Bohari ya Dawa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 19, 2025,na kueleza kuwa bidhaa
zote za afya 414 zenye thamani ya shilingi 100,182,390,897.40 zimekwisha sambazwa
na kusimikwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Amesema katika kipindi cha miaka minne Vituo vya kutolea huduma
za afya vinavyohudumiwa na MSD vimeongezeka na kufikia vituo 8,466 mwaka
2024/2025 kutoka vituo 7,095 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la vituo 1,371
ambapo ni ongezeko la asilimia 19.
" Ongezeko kubwa la vituo vya kutolea huduma za
afya vinavyopelekewa bidhaa na MSD lilikuwa kwenye zahanati ambapo vituo 1,102
viliongezeka na ndipo ambapo wananchi wengi wanapata huduma, "amesema
Amesema kuwa Bohari ya Dawa imeendelea kuhudumia vituo hivyo kupitia Kanda zake 10 zilizopo
Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya
na Iringa.
Kuhusu mafanikio ya MSD amesema
hadi kufikia tarehe 15 Februari 2025, imeendelea kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya katika vituo vya
kutolea huduma za afya na kwamba
hali ya uwepo wa bidhaa za afya ashiria 382 imeongezeka kutoka asilimia 42 mwaka
2021/2022 hadi asilimia 67 mwezi Februari, 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia
23.
"Hali ya utimizaji wa mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya umeendelea kuimarika
ambapo hadi mwezi Juni 2024, hali ya utimizaji wa mahitaji ulifikia asilimia 79," amesema
Mkurugenzi huyo pia ameeleza Mpango Maalum wa Usambazaji wa Mashine za Uchujaji damu kuwa Serikali inatekeleza mpango maalumu wa kuongeza upatikanaji
wa huduma za uchujaji wa damu ikiwa ni sehemu ya matibabu ya figo, hivyo kupunguza
gharama za huduma hiyo.
"Kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya
awamu ya sita, hadi kufikia mwezi Februari 2025, idadi ya mashine imeongezeka na
kufikia mashine 137 kutoka mashine 60 na hivyo kuongeza idadi ya hospitali zilizopokea
mashine kutoka Bohari ya Dawa kutoka hospitali 6 zilizokuwepo mwaka wa fedha
2021/22 na kufikia hospitali 15 mwaka 2024/25, "amefafanua.
Amesema uwekezaji huo umegharimu
kiasi cha shilingi bilioni 7.7.
Katika hospitali hizo ambapo, hospitali 11 zimeanza kutoa huduma na hospitali 4 zipo katika hatua
ya matengenezo.
Amezitaja baadhi ya hospitali zinazotoa huduma ni pamoja na Hospitali za Rufaa
za Mikoa ya Amana, Mwananyamala ,Temeke, Morogoro, Katavi, Tumbi, Chato, Sekoe
Toure na UDOM Hospitali.
Amefafanua kuwa Mkakati huo wa usambazaji wa mashine za dialysis unalenga kupunguza gharama
ambapo kwa sasa gharama zinazotozwa ni kati ya shilingi 200,000 na shilingi 230,000
na matarajio ni kuweza kupunguza na kuwa chini ya shilingi 100,000 kwa ‘session’
moja.
Mwisho
0 Comments