Uzinduzi wa mradi huo umefanywa rasmi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Daniel Mushi na kubainisha kuwa, mradi huo utafanya kazi nchini kwa muda wa miaka minne ambapo unagharimu Dollar Milioni Nne za Kimarekani (USD 4 Mil) sawa Bilioni 10 za Kitanzania ambazo ni kwa Nchi tatu za Tanzania, Uganda na Namibia.
Mushi amesema mradi huo utalenga maeneo manne muhimu ambayo ni pamoja na kuboresha mazingira ya walimu katika matumizi ya TEHAMA. Eneo lingine ni kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kutengeneza maudhui ya kufundishia kupitia zana za kidijitali ili wanafunzi wazitumie ilikutoa fursa wanafunzi mbalimbali kupata maeneo ya kujifunzia.
Ambapo eneo la Tatu ni kutengeneza kihunzi cha kupima weledi wa wanafunzi kwenye matumizi ya TEHAMA na eneo la nne ni kuongeza ushawishi wa kisera ili kupata sera bora zaidi za kuboresha matumizi ya TEHAMA katika kufundishia na kujifunzia.
Ameongeza kuwa Serikali inauona mradi huo kuwa na manufaa makubwa kwa sababu nchi ni kubwa, na wanafunzi waliopo vijijini wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa vitabu, jambo ambalo linaathiri masomo yao. Kupitia mradi huu, changamoto hiyo itatatuliwa, hivyo kuhakikisha uwiano wa fursa za elimu bora kwa wanafunzi wa mijini na vijijini.
"Mradi huu unamanufaa makubwa kutoka na nchi yetu ni kubwa na yenye kukua kwa maeneo mbalimbali hivyo TEHAMA itaenda kuboreshamazingira ya wanafunzi ikiwe wa mjini na vijijini.
Walimu wazuri watapatikana na kufundisha wanafunzi wengi zaidi. Ili linaenda kuiongezea nguvu Serikali katika malengo yake ya ukuaji wa TEHAMA." amesema Mushi.
Nae Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni ( UNESCO) nchini Tanzania, Michel Toto amesema mradi huo ni muhimu kwa Tanzania kwani unaenda kuboresha mazingira sahihi ya kujifunzia wanafunzi katika kukua Kidijitali.
Kwa upande wake, Naibu Msimamizi Mkuu wa Misheni kutoka Jamhuri ya Korea, Lee Seungyun, amesema kuwa mradi huu utawajengea watoto wa Kitanzania ujuzi unaohitajika katika soko la ajira linalohitaji maarifa ya TEHAMA, na hatimaye kuandaa Taifa lenye mustakabali mzuri wa kielimu.
Naye Mratibu wa Mradi wa KFIT kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Lina Rujweka, amesema utekelezaji wa mradi huo utahusisha wizara na taasisi mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya TAMISEMI, na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Rujweka ameishukuru Serikali kwa kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mitaala iliyoboreshwa, akisema kuwa sera hiyo imehimiza sana matumizi ya TEHAMA, hivyo mradi huu utatekeleza malengo na shabaha za Sera Mpya ya Elimu.
























0 Comments