Costantine Mathias, Simiyu.
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi, amewataka wananchi kutunza miradi ya Maji inayotekelezwa na serikali ili iweze kunufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa huku akisisitiza kuwachukulia hatua wale wote watakaohujumu miundombinu ya Maji.
Kihongosi ameyasema hayo leo, March 20, 2025, wakati akizundua Mradi wa Maji Oldmaswa uliotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini na Vijijini (RUWASA) Mkoani humo, kwa gharama ya shilingi Mil. 464.3 na utanufaisha wananchi 4220 kutoka Mitaa ya Mwahabi, OldMaswa na Nyangaka.
"Wananchi tunzeni miradi ya Maji na miundombinu yake, yoyote atakayechezea miradi hii atachukuliwa hatua Kali za kisheria...serikali ya Dk. Samia inajenga miradi ya Maji ili iwanufaishe wananchi, nasi tuna deni kubwa na kumlipa mwezi Oktoba Kwa kumpa kura za kishindo" amesema Kihongosi.
Awali Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Bariadi, Mhandisi Heri Magoti amesema utekelezaji wa Mradi huo ilianza mwaka 2024 kwa gharama ya shilingi Mil. 464.3 na inatarajia kunufaisha wananchi 4,220.
Ameeleza kuwa Mradi huo inatarajia kutoa huduma ya Maji safi na salama Kwa wananchi kutoka Mitaa mitatu ya Mwahabi, Oldmaswa na Nyangaka ambao mahitaji yao ya Maji kwa siku ni lita 147,700 na kwamba chanzo cha Mradi huo kinazalisha lita 180,000 kwa siku.
Diwani wa Kata ya Nyakabindi, Davidi Masanja ameishukuru serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea Mradi huo ambao umekata kiu ya wananchi kwa kuwatoa ndoo kichwani Wanawake.
"Tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa kutekeleza Mradi huu, zaidi ya Mil. 400 zimeletwa hapa Oldmaswa, sisi wananchi tunamshukuru sana sababu tangu Dunia iumbwe, viongozi mbalimbali wamepita lakini hatukupata Mradi kama huu, tunashukuru sana" amesema Masanja.
Edward Sumbuka, mkazi wa OldMaswa ameipongeza serikali kwa kukamilisha Mradi huo ili kuwaondolea adha Wanawake ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya Maji, huku akiwataka Wananchi kushirikiana kulinda miradi ya Maji na miundombinu yake.
Mwisho.


0 Comments