Header Ads Widget

NACONGO MKOA WA IRINGA WAMTUNUKU TUZO AIDAN MLAWA


Na Matukio Daima Media 

Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) mkoa wa Iringa limemkabidhi tuzo maalum mdau wa maendeleo kutoka wilaya ya Kilolo na mkoa wa Iringa, Aidan Mlawa, kutokana na mchango wake mkubwa katika kufanikisha shughuli za baraza hilo pamoja na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Tukio hilo limefanyika leo katika ukumbi wa Iringa Sunset Hotel ambapo mkutano mkubwa wa Nacongo mkoa wa Iringa umefanyika. 

Hafla hiyo imehudhuriwa na wadau mbalimbali wa mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa serikali, pamoja na wawakilishi wa sekta binafsi ambao kwa pamoja walishiriki kujadili mafanikio, changamoto na mustakabali wa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika mkoa huo.

Akizungumza kabla ya kumkabidhi tuzo hiyo, mwenyekiti wa Nacongo mkoa wa Iringa, Fidelis Filipatali, ambaye pia ni mjumbe wa Nacongo Taifa, alieleza kuwa Aidan Mlawa ni miongoni mwa wadau wachache waliotoa mchango mkubwa kufanikisha mkutano huo. 

Filipatali alifafanua kuwa Mlawa amekuwa mfano bora wa wadau wa ndani wanaotambua umuhimu wa kuendeleza sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kutegemea rasilimali za ndani badala ya kusubiri wafadhili wa nje pekee.

“Wakati tunapanga mkutano huu, tulikumbana na changamoto kubwa ya kifedha. 

Tulihitaji fedha kwa ajili ya maandalizi ya ukumbi, chakula, vitendea kazi na gharama nyingine za mkutano.


 Katika harakati za kutafuta wadau wa kutuunga mkono, mtu wa kwanza kabisa tuliyemfikia ni Aidan Mlawa. Mlawa hakusita, alitupokea vizuri na mara moja aliahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni mbili (2,000,000),” alisema Filipatali huku akipigiwa makofi na washiriki wa mkutano huo.

Alisema kuwa mbali na ahadi hiyo ya kifedha, Aidan Mlawa alitoa zaidi ya fedha kwani alitoa faraja na hamasa kubwa kwa viongozi wa Nacongo mkoa wa Iringa kuendelea kusimamia maandalizi ya mkutano huo kwa nguvu na ari kubwa.

 Filipatali alisisitiza kuwa mara nyingi mashirika yasiyo ya kiserikali hukumbwa na changamoto za kifedha, lakini ni nadra sana kupata wadau wa ndani wanaoonyesha nia na kujitoa kama alivyofanya Mlawa.

“Mlawa ametufundisha jambo kubwa, kwamba tunaweza kujitegemea na kuaminiana sisi kwa sisi kama wadau wa maendeleo wa ndani ya nchi yetu. 


Kupitia msaada wake na faraja aliyoitoa, leo tupo hapa Sunset Hotel tukifanya mkutano huu muhimu,” aliongeza mwenyekiti huyo.

Aidha, Filipatali alitaja baadhi ya wadau wengine waliotoa mchango wao kufanikisha mkutano huo, akiwemo mmiliki wa Iringa Sunset Hotel aliyetoa ukumbi kwa gharama nafuu, benki ya NBC ambayo ilitoa mchango wa kifedha, Kampuni ya Maziwa ya Asas ambayo ilisaidia vinywaji na vitafunwa kwa washiriki, pamoja na chombo cha habari cha Matukio Daima Media ambacho kilihakikisha mkutano huo unapata umaarufu na kuwafikia wananchi wengi wa mkoa wa Iringa na nje ya mkoa huo.

Kwa upande wake, baada ya kupokea tuzo hiyo kutoka kwa Msajili Msaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mkoa wa Iringa, Bi. Saida Mgeni, Eliasa Ally ambaye alimpokea tuzo hiyo kwa niaba ya Aidan Mlawa, alisema kuwa Mlawa si mdau wa maendeleo wa Kilolo pekee bali ni mdau wa maendeleo kwa mkoa mzima wa Iringa na hata nje ya mkoa huo.

“Mlawa ni mtu wa watu. Amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na mashirika, vikundi vya kijamii, taasisi za serikali na hata sekta binafsi kuhakikisha maendeleo ya kweli yanafanyika, hasa katika maeneo ya elimu, afya, kilimo na miradi ya vijana.


 Anaamini kuwa maendeleo hayaletwi na serikali pekee bali ni jukumu la kila mmoja wetu, hususan sisi wananchi wa kawaida kushirikiana kwa hali na mali,” alisema Eliasa Ally kwa niaba ya Mlawa.

Aliongeza kuwa Mlawa ni miongoni mwa wafanyabiashara wa kizalendo wanaoamini katika uwekezaji wa maendeleo ya jamii. Alisema mbali na mchango wake kupitia Nacongo, Mlawa amekuwa na miradi mingi ya kijamii katika wilaya ya Kilolo kama vile kusaidia shule za msingi na sekondari kwa vifaa vya kujifunzia, kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa, kusaidia vituo vya afya kwa vifaa tiba, pamoja na kuwezesha vijana na wanawake kupata mitaji ya kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi.


“Kwa Mlawa, kila jambo linalogusa jamii ni jambo lake. Anajiona kama sehemu ya jamii na kila anapopata fursa anahakikisha anarejesha sehemu ya mafanikio yake kwa jamii iliyomzunguka. Hii ni dhana ya maendeleo shirikishi ambayo kila mmoja wetu anatakiwa kuiga,” aliongeza Eliasa.

Washiriki wa mkutano huo walipongeza uongozi wa Nacongo mkoa wa Iringa kwa kutambua mchango wa watu wa ndani kama Mlawa, wakisema kuwa hatua hiyo itaongeza hamasa kwa wadau wengine kushiriki katika kuleta maendeleo ya jamii.

“Zamani tulizoea kuona mashirika yasiyo ya kiserikali yakitegemea misaada kutoka nje ya nchi pekee, lakini kupitia mfano wa Mlawa na wadau wengine wa ndani, tumefahamu kuwa hata sisi wenyewe tunaweza kuwa sehemu ya suluhisho kwa changamoto zetu,” alisema mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Bi. Agness Kihaga kutoka shirika la maendeleo ya vijana wilaya ya Mufindi.

Tuzo hiyo ya heshima kwa Aidan Mlawa imekuja wakati ambapo mkoa wa Iringa unatekeleza mpango mkakati wa kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi na wadau wa ndani katika kuchangia maendeleo ya jamii. 

Mpango huo unaungwa mkono pia na serikali kupitia ofisi ya msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushirikiano kati ya mashirika hayo, serikali na sekta binafsi ili kufanikisha maendeleo endelevu ya mkoa wa Iringa.

Kwa kumalizia, mwenyekiti wa Nacongo mkoa wa Iringa, Fidelis Filipatali alitoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wa Aidan Mlawa na kuhakikisha kila mmoja anatoa mchango wake kulingana na uwezo wake kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla.

“Nacongo tunamshukuru sana Mlawa na wadau wote waliosaidia kufanikisha mkutano huu. Ni imani yetu kuwa huu ni mwanzo wa safari ndefu ya mafanikio kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na maendeleo ya mkoa wetu wa Iringa,” alihitimisha Filipatali.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI