Mmiliki wa timu ya Muembe Makumbi City, Ussi Salum Pondeza amejumuika na wachezaji, viongozi na mashabiki mbali mbali kwenye Iftar maalum iliyoandaliwa na timu hiyo, huko Mbweni, Zanzibar.
Alhaj, Pondeza amewasisitiza wachezaji hao kuendelea kujituma na kuipambania timu hiyo ili kufikia malengo waliyojiwekea ikiwemo kubeba ubingwa.
Pondeza, ambae ni Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, amesema furaha yake ni kuona vijana wanajiajiri kupitia fani ya michezo ambayo imepanda hadhi kubwa kwa kipindi cha hivi karibuni.
Pia, amewaomba kuzingatia, nidhamu, uvumilivu na kujitoa ili kufikia matarajio ya mashabiki wengi wa timu hiyo.
Baadhi ya viongozi na wachezaji wa timu hiyo ya Muembe Makumbi City wameahidi kuendeleza ari na hamasa ili kuunga mkono jitihada za mbunge huyo.
Wamesema ligi ni ngumu na imekuwa na ushindano mkubwa lakini malengo yao ni kuhakikisha wanabeba ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu ya Muembe Makumbi City kuandaa iftar maalum kwa wachezaji na viongozi wake.
Mpaka Ligi Kuu inasimama kupisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, Mumbe Makumbi City inaongoza ligi kwa alama 41 ikifukuzana na mpinzani wake wa karibu timu ya Mlandege yenye alama 38, timu zote zikiwa zimebakisha michezo 10.
0 Comments