Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, amechangia fedha kiasi cha shilingi million moja kwa ajili ya ujenzi unaoendelea katika kanisa la Baptist Mjele na shilingi million moja nyingine kwa ajili ya kanisa la Moravian Ushirika wa Mjele ambao pia wanaendelea kujenga kanisa jipya kwa ajili ya kuabudia.
Baada ya kushiriki ibada katika makanisa hayo kwa nyakati tofauti, Mbunge Njeza amewaomba viongozi na waumini kuendelea kuliombea Taifa na kuombea uchaguzi ili kupata viongozi bora kwa mwaka huu 2025.
Katika ziara hiyo, mbunge aliambatana na Mchungaji wa kanisa la Baptist Alfred Rojas kutoka Shigamba Ilembo, amewaasa wananchi na waumini kuendelea kuwaombea viongozi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Mchungaji wa kanisa la moravian Tanzania jimbo la kusini magharibi ushirika wa Mjele Japhet Amoni Mwalembe, amesema Serikali inahitaji kuwa na viongozi wenye nia ya kweli kuwatumikia wananchi bila udanganyifu na kumshukuru mbunge wa Mbeya vijijini kwa kuwa na ahadi za kweli ikiwemo kuwasilisha mchango na sadaka yake ya shilingi million moja ili kuwaunga mkono kwenye ujenzi na utekelezwaji miradi mbalimbali ya kanisa hilo.
Wakizungumza baada ya ibada, baadhi ya waumini wameeleza utayari wao kuchagua viongozi bora mwaka huu 2025 ili kuendeleza kazi kwa kutatua kero ambazo zimesalia ikiwemo ubovu wa barabara ya Mbalizi Chang'ombe hadi Mkwajuni na Makongolosi, umeme kutosambaa kwenye kijiji chao cha Mjele kutokana na ukosefu wa nguzo na ukosefu wa ajira kwa vijana wao.
Wananchi wa kijiji na kata ya Mjele wamewataka viongozi wa sasa na wajao kuhakikisha wanapambana kupigania mabadiliko zaidi ya kijiji chao kama ilivyofanyika kwa baadhi ya miradi iliyotekelezwa ikiwemo maji ambayo sasa yanapatikana, elimu hasa ya sekondari kujengwa katani hapo na umeme ambao umefika kijijini kwao licha ya kutosambaa vitongojini.
0 Comments