Na Shomari Binda-Musoma
MATUKIO ya ukeketaji yameshuka mkoani Mara kwa asilimia 8 kutoka asilimia 10 kwa wasichana na wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49.
Kushuka kwa kiwango hicho kumetokana na juhudi za wadau mbalimbali wanaopambana na matukio ya ukatili wa kijinsi kwa kutoa elimu mkoani Mara.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kupinga Ukatili wa Jumuiya ya Wanawake ( UWT) mkoa wa Mara Rhobi Samwelly machi 20,2025 wakati akitoa taarifa kwenye kikao cha baraza la jumuiya hiyo.
Amesema kwa mujibu wa utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na viashiria vya malaria ( TDHS-MIS)ya mwaka 2022-2023 unaonyesha kiwango hicho kushuka.
Rhobi amesema licha ya vitendo vya ukatili wa aina ya ukeketaji kushuka bado yapo matukio mengine ya ukatili kama vipigo,ubakaji ndoa za utotoni,mauaji na manyanyaso ya kutelekezwa na kuomba kuongezwa juhudi zaidi za kupambana na matukio hayo.
" Napenda kuwaomba viongozi wanawake ndani ya jumuiya ya UWT na wadau mbalimbali wanaopambana kupinga ukatili wa kijinsia kwa uratibu wa serikali kuendeleza juhudi za kukabiliana na ukeketaji na aina nyingine za ukatili.
" Hili ni jukumu letu sisi viongozi kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yetu ikibidi kupaza sauti kwa wasioweza kupaza sauti",amesema.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa amesema jumuiya hiyo mkoa wa Mara imeshiriki kukemea ukatili wa kijinsia wa aina zote kwa kutoa taarifa na kushirikiana na wadau mbalimbali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Mara Nancy Msafiri amempongeza na kumshukuru Rhobi Samwelly kwa jitihada na juhudi zake za kupambana na matukio ya ukatili.
Amesema kupitia kituo chake cha nyumba salama kilichopo wilaya ya Serengeti na Butiama amewasaidia na kuwahifadhi wahanga watoto wa kike na wasichana wanaofanyiwa na kukimbia vitendo hivyo.
Nancy amesema UWT mkoa wa Mara itaendelea kutoa ushirikiano wote kuona juhudi za kupambana na masuala ya aina zote za ukatili zinafanikiwa.
0 Comments