Header Ads Widget

KITUO CHA AFYA HIMO CHAZINDUA HUDUMA YA MIONZI.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI. 


KITUO cha Afya Himo kilichopo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro kimezindua huduma ya mionzi (X-Ray), ambayo itawawezesha wananchi wa wilaya ya Moshi na maeneo jirani kupata huduma hiyo kwa urahisi na kwa gharama nafuu.


Huduma hii imeanzishwa baada ya jitihada za serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoa fedha kwa ajili ya miundombinu ya Afya ikiwemo tiba mionzi, ambayo iligharimu shilingi milioni 200.



Akizungumza kuhusu huduma hiyo, mtaalamu wa teknolojia ya mionzi katika kituo hicho, Abdon Novat, alisema vifaa vya kisasa katika kituo hicho vitarahisisha utoaji wa huduma hiyo ambayo itasaidia kubaini magonjwa na matatizo ya kiafya kwa haraka na kwa usahihi.


Kwa upande wake, Kaimu Mfawidhi wa Kituo cha Afya Himo, Dkt. Ahmed Ulimwengu, alieleza kuwa pamoja na huduma ya X-Ray, kituo hicho kinatoa huduma ya kinywa na meno, ambapo kwa siku wanahudumia wagonjwa 12, na kwa mwezi wanahudumia wagonjwa 430. 



Dkt. Ulimwengu aliongeza kuwa huduma ya tiba mionzi itaendelea kutolewa kadri wananchi watakavyopata uelewa na kuendelea kutembelea kituo hicho kwa ajili ya matibabu.


Alimshukuru Rais Samia, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, pamoja na Diwani wa Kata ya Makuyuni kwa juhudi zao za kuhakikisha upatikanaji wa vifaa hivyo.


Dkt. Charles Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, ambaye alishiriki kwa karibu katika upatikanaji wa mashine ya X-Ray, alisema kuwa hatua hii ni muhimu kwa wananchi kwani itapunguza gharama na muda wa kwenda hospitali za wilaya, hospitali za rufaa, au vituo binafsi ambapo huduma za X-Ray ni ghali zaidi.



"Huduma hii imeanza kutolewa hapa kwenye Kituo cha Afya Himo, na gharama yake ni nafuu mara mbili ya ile ya vituo binafsi. Naendelea kuwahimiza wananchi kutumia huduma hizi muhimu, bora na za gharama nafuu, Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ya miradi ya afya, elimu, barabara na maji ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)," alisema Dkt. Kimei.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya Wananchi wa Himo, walishukuru kwa ujio wa huduma hiyo, wakieleza kwamba hapo awali walilazimika kufuata huduma hiyo katika vituo binafsi kwa gharama kubwa au kwenda mjini Moshi, lakini sasa wamerahisishiwa huduma hiyo karibu na nyumbani kwao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI