N. Kwiyeyu Singu, Nzega.
Katika mwendelezo wa makala iliyopita, makala hii itajikita zaidi upande wa utamaduni wa watu wa Tabora (Wanyamwezi) na nitagusia kidogo siasa kihistoria.
Nianze na hili la historia ya Tabora, ni mkoa ambao umekuwa maalufu sana hapo nyuma ndani na nje ya Tanzania ktk medani ya siasa ya Tanzania.
Sisi wakati tukiwa vijana wadogo, ktk taarifa za habari za kimataifa ilikuwa huwezi kuisikia Tanzania kisiasa bila kuitaja Tabora, wanasiasa wengi wa Tanzania wameibukia Tabora akiwemo Mwalimu Nyerere na wengine wengi tu.
Halikadhalika harakati za ukombozi zimefanyika zaidi katika Mkoa wa Tabora.
Hata dira (Azimio la Arusha) ya taifa letu ilisukwa hapa hapa Tabora.
Harakati hizo kwa kiasi kikubwa ziliongozwa na akina Fundikila, Kasanga Tumbo, Kasela Bantu, Zuber Mtemvu, Mwalimu Nyerere, Bibi Titi na wengine pia.
Lakini cha kushangaza taswira hii ya wanyamwezi ktk medani za kisiasa ilianza kupotea miaka ya kuelekea 2000, siasa ya nchi yetu ikageuka kuwa soko la walaguzi wa kununua kura, ikawa kila mwenye shilingi zake au hata za kupewa na marafiki zake aliweza kwenda jimbo lolote analoona anaweza kununua uongozi.
Mfumo huu wa kununua uongozi ililetwa zaidi na akina Lowasa na Lostam wakati wa harakati za Jakaya Kikwete kuwania urais.
Katika uchambuzi wangu nilisema nitaanzia alipoishia Mzee Kahumbi, kwa kuwa ndiyo wakati wa vuguvugu la mabadiliko likiwa limepamba moto zaidi.
Wakati huo vyama vya siasa vya upinzani vilikita mizizi yake hadi vijijini, wanasiasa wa upinzani kama Mzee John Cheyo, Mtikila, Mrema, Profesa Lipumba na wengine walijenga ushawishi mkubwa sana ambao mimi binafsi tangu kijana mdogo na hadi sasa sijawahi kushuhudia tena ushawishi kama ule.
Kwa mfano kata moja tu iliyoko vijiji kama Mwangoye, wazee maarufu kama Mzee Makutano, Mzee Said "kidevu" (Mwarabu), Mzee Mishinga na wengine wengi walijitosa ktk vyama vya upinzani NCCR, CUF na UDP ya hofu yoyote.
Na haikuwa wazee tu, vijana wengi ndio walioshiliki zaidi siasa za vyama vya upinzani enzi hizo.
Lakini cha kushangaza ni kwamba, sasa hivi wanyamwezi hawa hawa waliosifika kama taswira ya siasa za Tanzania, siyo tena kama wale wazee wetu akina Fundikila, Kaselabantu, Kasanga Tumbo na akina Samweli Sitta.
Sasa hivi ni wanyamwezi sampuli ya akina Profesa Kapuya aliyekuwa tayari kumleta Mmasai 'Lowasa' na kumpa uchifu wa Wanyamwezi.
Hata mijadala yetu sasa siyo ile inayozungumuzia masuala ya nchi na maslahi yake, hakuna mijadala ya msingi bali majadiliano yanabaki ktk ngazi ya kuangalia sura ya mtu, mavazi yake, kabila lake, dini yake, urefu wake, ufupi wake, unene wake, uwezo wake wa kuongea kiingereza, ukasuku wake na uhodari wake wa kuwashawishi akina Lostam kuja kuwekeza miradi ya kunyonya kodi za wananchi!
Hatuingii ndani zaidi kuchunguza, sura nzuri ina nini ndani yake, mavazi yanayovutia na yenye bei kubwa yanatunufaisha nini?
Urefu wa mtu unamaanisha urefu wa akili yake, na ufupi wa mtu unawakilisha ufupi wa akili yake?
Uwezo wa kuongea kiingereza unasaidia kuleta maendeleo ya wananchi au unasaidia kufanya ufisadi na kuibia kodi za wananchi?
Ni kipi kinamfanya mtu awe wa maana na mwenye thamani kubwa kwa wananchi na taifa lake?
Ni mavazi, kiingereza, kabila, maumbile ya mwili au fikra pevu iliyonolewa kwa njia mbalimbali?
Je, ni uzalendo, uwajibikaji, upeo wa kuona mbali, kipaji cha kuchambua mema na mabaya kwa manufaa ya wananchi?
Kuwa kiongozi wa kisiasa siyo jambo la mchezo ambalo kila mtu anaweza kuwa kiongozi wa watu.
Huu ni ukweli ambao ingawa ni mchungu lazima usemwe, na kwa kuelekea uchaguzi wa madiwani na wabunge na hata Rais wa nchi unahitajika usemwe zaidi na mara kwa mara.
Hii ndiyo sababu iliyofanya kuzaliwa kwa utamaduni mpya ktk mkoa huu wa wanyamwezi, utamaduni huu umeufanya mkoa wa Tabora ubaki ulipo bila kusonga mbele kimaendeleo, na haya alikuja kuyathibitisha Rais Dk Magufuli pele mkoani aliposema, "Tabora mnamajungu mno, acheni majungu mjenge mkoa wenu..."
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, pia naye alikuja Wilaya ya Nzega akawashangaa viongozi wa kisiasa wakuvutana na watendaji wa serikali na kufanya maendeleo yasimame. Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Ally Bashiru, naye alifika na kushangaa, yeye akaenda mbali na kusema, viongozi wa CCM pamoja na wanasiasa hakuna hata mmoja mwenye sifa nzuri, wote wameshiriki kutengeneza migogoro ya kuwahujumu wananchi.
Waziri Jafo naye alipita mule mule, kubwa zaidi ni pale Rais Dk Magufuli alipoamua kuirudisha fedha ya ujenzi wa stand ya mabus Nzega kutokana na wanasiasa kuvutana nani awe mkandarasi, kwa zaidi ya miezi 3.
Haya ndiyo madhara ya huu utamaduni mpya wa kuangalia sura ya mtu, dini yake, kabila lake, uwezo wake wa kuongea kiingereza, ukasuku na uhodari wake wa kuwashawishi matajiri wampe fedha za kuja kununua kura.
Sasa wanyamwezi hawaingii kiundani kuchunguza sura nzuri ina nini ndani yake, pesa anazowapa atazirudishaje akiingia madarakani au atawanyonya kodi zao nk.
Nimegusia masuala haya kwa upana zaidi kwa kugusa mkoa na taifa kutokana na mazingira ya hoja, lakini uchambuzi unahusu Jimbo la Bukene ambalo kwa sasa linaongozwa na Mbunge Seleman Zedi, ambaye amechuku takribani ya miaka 20 sasa.
Tumezunguka karibu kata zote za jimbo la Bukene na kufanya uchambuzi wetu juu ya miaka yote ya uongozi wa Seleman Zedi na kubaini mambo kadhaa ambayo ni muhimu yaeleweke.
Yapo mambo yanaihusu serikali ambayo yalihitaji msukumo wa diwani na mbunge kwa kuwasilisha mahitaji ya wananchi, na yapo ambao yanamhusu mwanasiasa mwenyewe kuyafanya.
Sasa uchambuzi huu unagusia mazuri na madhaifu ya serikali, lakini hasa mazuri na madhaifu ya mwanasiasa ktk jimbo analoliongoza.
Kutikana na mlolongo wa mambo mengi tuliyoyapata, si yote tutayaweka wazi kupitia makala hizi na kwa wakati huu, si tu kwa jimbo la Bukene bali pia majimbo yote tutafanya hivyo, yale yanayotakiwa kuyaweka wazi sasa ndiyo haya tunaendelea kuyaweka wazi ili wananchi wayaelewe, na ndiyo jukumu letu kuwaelimisha wananchi na kufanya nao mijadala mbalimbali na hatimaye kuweza kupata mwafaka mwema.
Na kuelekea kuhitimisha uchambuzi wetu kwa jimbo la Bukene, maswali mengi tumekuwa tukiulizwa na wadau wa maendeleo pamoja na wananchi kuwa ni je, Zedi ni Kiongozi mwanasiasa?
Au Je, Zedi ni Kiongozi Mtendaji?
Au Zedi ni mtu tu aliye kwenye nafasi hiyo ya uongozi bila kuwa na sifa hizi mbili, yaani uwanasiasa or utendaji?
Makala ijayo itajaribu kuyajibu maswali haya kupitia uchambuzi wa kina juu ya sifa na vigezo ktk nafasi husika.
Itaendelea....
Kwiyeya Singu. 0784977072
0 Comments