Header Ads Widget

JIMBO LA BUKENE SEHEMU YA TATU...


Kuna dhana kwamba itikadi nchini imekufa, si kwa Itikadi ya CCM ya Ujamaa wala kusotokulia ya Chadema na vyama vingine, zimezikwa na hazitafufuka tena.

Itikadi iliyopo siku hizi ni itikadi ya ubepari, itikadi hiyo haijazivaa nchi kama Tanzania tu lakini imeimeza takrabani dunia nzima hasa nchi za Afrika na Ulaya magharibi ikiwemo Marekani ambaye ndiyo mwasisi mkuu.

Waswahili husema, "Mzigo mzito mpe Mnyawezi", huu ni msemo maarufu nchini ulioibuliwa 'bila shaka wakati wa biashara ya utumwa, (ukoloni)', unaomaanisha kwamba 'mzigo mzito mtwishe Mnyamwezi anaweza kuhimili' tena kwa woga na hofu kubwa hata kama anaumia, atafika nao mbali.

Wilaya ya Nzega, kama nilivyotangulia kusema kwenye makala zilizopita, ni Wilaya ambayo inaogelea ktk dhiki za aina lukuki ukilinganisha na Wilaya za jirani ambazo zimetokana na Wilaya hii ya Nzega kama Kahama na Igunga.

Kuanzia elimu, uchumi, siasa zake na hali ya kitamaduni kwa ujumla temkuwa nyuma sana.

Yaani " Wanyamwezi" tunajulikana kwa shida zilizo nje ya uwezo wetu hadi shida za kujitakia wenyewe kama zile za kuruhusu kuwa na viongozi na wanasiasa mafisadi, wabovu wa hovyo.

Lakini huenda kitu kibaya zaidi, na kinachooudhi, tunatuhumiwa na watu wengi wakiwemo wanasiasa wa upinzani kila wanapokuja hapa Nzega kwamba, uwezo wetu wa kufikiri ni hafifu. 

Ndiyo sababu zipo shida nyingi za kujitakia hapa Nzega kiasi cha kufanya maendeleo yasipae kama ilivyotazamiwa na maisha ya wananchi kuwa duni.


Kuna msemo kwamba "Anayepambana ndiye anayeshinda."

Kupambana hapa maana yake ni kujibu changamoto za wakati husika kwa kutumia majibu sahihi yanayojibu alama za nyakati.

Katikati ya tuhuma hizi, wapo wasomi ambao ni wazawa wa hapa Nzega ambao walijaribu kupambana na mwisho wa siku wakajikuta wakiwa matatani na hata kulaumiwa na wananchi wenyewe.

Hawa walijitahidi kuitetea jamii yetu ya Nzega dhidi ya viongozi mafisadi, wabovu na wa hovyo.

Kwa mfano, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Nzega, Dkt. Hamis Kigwangalla, alijitolea maisha yake kupambania fedha zilizotakiwa kutolewa na Mgodi wa Nzega, ambazo kwa kiasi fulani zilikuwa zinatafunwa na viongozi serikalini bila kufanyiwa maendeleo katika jamii ya wana wa Nzega.

Lakini Dk. Kigwangalla alipigwa mabomu na Polisi na vile vile alipigwa vita na viongozi serikalini, kuanzia Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Viongozi wa CCM, Madiwani ambao walipata nguvu kutoka kwa Bashe aliyekuwa akiwania Jimbo la Nzega.

Halikadhalika, Elias Machibya, ambaye kwa kipindi hicho akiwa Chadema - kabla hajahamia CCM, naye alipambana na uonezi wa viongozi uliofanywa kwa wananchi wa Jimbo la Bukene, huku Mbunge wao Seleman Zedi na viongozi wa chama na serikali wakiwa hawajali kabisa, naye aliambulia lawama.

Kwenye makala ya kwanza nilitoa historia ya Tabora na watu wake (Wanyamwezi) kwa jinsi walivyokuwa maarufu katika kupigania ukombozi wa nchi yetu ya Tanzania (Tanganyika ya wakati huo), niliwataja wanyamwezi wachache kama Chief Fundikila, Kaselabantu, Kasanga Tumbo na baadaye akina Samwel Sitta.

Baada ya hao, Tabora ilibadili kabisa historia yake na kuwa ya hovyo, sasa tumekuwa watu wa majungu na fitina na tukitengeneza viongozi madikteta au kuruhusu uonevu wa viongozi mafisadi.

Zipo tuhuma mbalimbali wanazotuhumiwa viongozi wa kisiasa katika majimbo haya ya Nzega, kwa upande wa Bukene ambako bado tuko tukichambua na kujadili uingozi wa Jimbo, Mbunge wa jimbo hili, Seleman Zedi, anatuhumiwa kuwafanyia mpango wa kuwahamisha watumishi wa serikali (watendaji na waalimu) waliopo ndani ya Jimbo wale wanaonesha kutokubaliana naye kimawazo, kiutendaji ktk amri au utashi wake binafsi wa kisiasa.

Hata kwa wananchi anaowafadhili vitu vidogovidogo anatuhumiwa kuwanyang'anya pale inapoonekana watu hao hawamuungi mkono.

Kwa mfano pale Bukene mjini, baada ya kuonekana wananchi wa pale hawajampe kura nyingi alikwenda kufumua kibanda na kusambaratisha kijiwe cha kahawa alichokifadhili vitu vidogovidogo (viti, vyombo nk) 

Tuhuma zingine ni kwa watendaji wa chama ngazi ya kata na matawi, huwanyang'wa vyombo vya usafiri alivyowapa, na kutishia kuwaondoa kwenye nafasi zao za uongozi.

Hayo na mengine mengi ambayo sitayataja kwenye makala haya kutokana na muda, lakini inatosha kuonesha jinsi viongozi wa kisiasa wa sasa walivyo.

Hizi ndizo siasa za Nzega kwa sasa.

Kusema kwamba 'wanyamwezi tulikuwa na nguvu ya kupigania uhuru na haki, ila sasa hatuna nguvu hiyo' ni wazi kwamba tunakiri kuwa tumetupwa nje ya ulingo wa siasa za Tanzania, ambazo kimsingi asilimia 90 zimeasisiwa katika Mkoa huu wa Tabora.

Hatuko tena kwenye ule ulingo wa watu wanaopigana na changamoto zao na kuzishinda.

Hata wale walioonyesha utashi wa kupambana na ufisadi, akina Dkt. Kigwangalla nao wamenyosha mikono yao.

Ni sawa na kusema kwamba, kwa sasa uwezo wetu ni kuwatazama watu wengine kama wakurya wa Mara, wachaga wa Arusha, wasukuma wa Mwanza na wanyantuzu wa Shinyanga ya kale wanaoonyesha kupambana na changamoto na kufaidika japo kidogo na ushindi wanaoupata.

Kama wewe Mnyamwezi unaikumbuka historia nzuri ya wazee wetu niliowataja hapo juu, ni vema ujua kuwa ni wajibu wetu kukazana bila kupoteza muda wa kuwalaumu wengine kana kwamba wamezishika akili zetu.

Jamii inayokumbuka magumu ya kisiasa na kiuchumi, na mema iliyopitia, na inayoyatazama magumu, kwa vitendo  inanuiya kwa dhati kwamba magumu hayo yasitokee tena kamwe katika uchaguzi ujao na chaguzi nyingine huko mbele.

Ni vema jamii ianze kukataa kuwa wafungwa wa historia bali historia iwe imeifundisha jamii mbinu mpya.

Hata kama sisi (Nzega) ni duni, lazima tujue ni kwa sababu tumefanywa hivyo na wengine, lakini  isifanye kukwepa kuwajibika.

Ni kweli kwamba hasara ya kihistoria ya siasa hizi za hovyo, ambazo zilianza kumea zaidi miaka ya 90 kuelekea 2000 hadi sasa, siasa hizi zimeacha na kuendelea kujeruhi na kusababisaha vidonda.

Lakini vidonda vinaweza kupona, tunapaswa kujua kuwa, hata historia chungu inaweza kuwa mwalimu bora, badala ya kuganga majeruhi jamii inapaswa kuweka vigingi kuzuia hali hiyo.

Makala iliyopita ilihoji ikiwa Mbunge Seleman Zedi ni mwanasiasa, Kiongozi au ni mtu aliye kwenye nafasi ya uongozi wa kisiasa ?

Maswali haya huenda yakapata majawabu yake katika makala ijayo...


Kwiyeya Singu. 0784977072

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI