Header Ads Widget

JIMBO LA BUKENE SEHEMU YA MWISHO


Makala iliyopita ilihitimisha na swali linalohoji kwamba "Seleman Zedi ni Mwanasiasa, Kiongozi au ni Mtu aliye katika nafasi hizo?"

Kabla ya kujibu swali hili, nianze kwa kutaja changamoto jumuishi zinazotatiza maendeleo ya kijamii.

Kwanza suala la Rushwa na Ufisadi ambalo limebaki kuwa agenda mtambuka katika Jamii na hata katika nchi yetu ya Tanzania.

Ni wazi kwamba kama unataka kutoa maelezo ya kwa kiasi gani tumekwama au kudumaa kimaendeleo ni lazima uhusishe madhila ya rushwa na ufisadi kila eneo la nchi hii ingawa mjadala wangu unajikita zaidi eneo la Nzega.

Ni maelezo gani mtu anaweza kutoa kwa nini vijiji na mitaa yetu katika mji ni ya vumbi na haipitiki wakati inawezekana kabisa kuchonga barabara huko vijijini tena kwa viwango vya moramu, na mjini katika kiwango cha juu kwa kutumia malighafi rahisi na gharama nafuu sana kama saruji au mawe?

Hakuna mhandisi wa ujenzi asiyejua kwamba saruji inaweza kutumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara hususan za mitaa na zikatumika kwa miaka nenda rudi bila ya matatizo yoyote.

Huko vijijini vijiji vingi havipitiki wakati wa masika na hata kiangazi, huku mjini vile vile mitaa yetu mingi haipitiki.

Ukichunguza utagundua ni ufisadi na utapeli wa kutumia kalamu, ufisadi ni mkubwa na fedha inayobambikwa serikali ni kubwa sana na inakuwa hivyo zaidi kutokana na rushwa na ufisadi.

Juzi tu tumeshuhudia mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati anafungua stand ya ma-bus Nzega, bilioni 4.2 tuliambia imetumika kujenga stand lakini ukiangalia fedha inayosemwa kutumika (bilioni 4.2) na kilichojengwa pale unaweza kutamani kulia.

Huo ni mfano mmoja tu kati ya mambo ya hovyo wanayofanya wanasiasa wetu hapa Nzega.

Mfano wa pili ni kwenye taa za barabarani, tunalazimishwa kuzinunua kwa bei ya serikali ambazo ni zaidi ya mara tatu ya taa hizo hizo za solar zinazowekwa katika majumba ya watu binafsi.

Tulipokuwa tunazungumuza na wananchi wa jimbo la Bukene, kati yao wengi walisema hawaoni anachokifanya mbunge wao Seleman Zedi, na kwamba wanatamani kuona mtu mwingine ambaye atakuwa makini na anayezijua shida na mahitaji ya wananchi kimaendeleo.

Wanasema mbunge wao Zedi hawajawahi kusikia amepeleka kero zao, wala kujenga hoja bungeni inayohusiana na wananchi wake inayohusu maendeleo, na kama aliwahi lakini hawakumbuki alizungumzia nini ikiwa changamoto zao zimebaki kuwepo miaka yote.

Ni kweli kwamba wabunge wengi wanakumbwa na hali ya kutoyajua majukumu yao au kuyapa mgongo majukumu hayo na kuvaa koti la serikali kwa kuyafanya majukumu (hayo ya serikali) kuwa ndiyo yao ya kibunge.

Kwa mfano barabara, zahanati, hospital, madarasa na taa za barabarani, ni mambo ambayo ni wajibu wa serikali kuyafanya, hivyo hata asingekuwepo mbunge au diwani mambo hayo yangefanyika tu kwa kuwa ni mpango wa serikali kufanya kwa wananchi.

Mara nyingi serikali kwa mfano inapoleta gari la wagonjwa, au kujenga zahanati, kuweka taa za barabarani, siku ya kukabidhi, mbunge anavizia awepo na kutumia tukio hilo kama ni yeye kafanikisha, wakati mwingine mbunge eti anakabidhi gari la wagonjwa ktk kituo fulani cha afya!?

Nimeona nitangulie na hayo hapo juu kama sehemu ya hitimisho la makala hii, lakini katika kujubu swali la kama Seleman Zedi ni mwanasiasa, kiongozi au laa, nitaanza kwa kutaja kwanza sifa za kiongozi ni zipi kwa ufupi ili kuona kama Zedi ni mwanasiasa au sio mwanasiasa.

Moja ya sifa za kiongozi ni kuwa na falsafa na aiweke wazi kwa wananchi anaowaongoza juu ya anachokiamini, yaani anaamini nini kuhusu maendeleo na maana yake? Na kwamba ana maono gani katika kuyafikia maendeleo hayo?

Seleman Zedi ni mbunge wa miaka mingi sasa takribani miaka 20 sasa aliyoongoza kama mbunge, kwa vyovyote vile kama angekuwa na falsafa inayohusu maendeleo naamini angekuwa ameipambania Bukene ikawa kituo cha mazao ya kibiashara na kutengeneza fursa kwa wakulima (wananchi) za kibiashara au kiuchumi, Bukene na maeneo mengine mahususi kama Itobo na Mwamala.

Pale Bukene mjini pana fursa ya Treni inapita pale, lakini pia barabara inayotoka Tabora kwenda Kahama, Bukene kwenda Shinyanga na ile ya kuja mjini Nzega.

Magodauni ya kikoloni yaliyopo pale hayafanyi kazi iliyofanyika miaka ya nyuma, wakati yangetumika kuhifadhi mazazo ya wakulima na pia kujenga viwanda vya kuchakata mazao na kuyapa thamani na kuyasafirisha kwenda sokoni.

Tatizo la wanasiasa wengi si wabunifu, wanaweza kutamka na kuahidi watafanya hili na lile na mara baada ya kuchaguliwa wanasahu kila kitu, kumbe wanakuwa wanawahadaa wapiga kura tu.

Hakuna kipaumbele cha maana kutoka kwa mwanasiasa zaidi ya kuahidi watafanya hili na lile bila hata kuainisha watayafikia vipi hayo wanayoyaahidi, matokeo yake muda wa uchaguzi unapowadia wanaanza kukimbizana na serikali kwenye miradi yake ili waonekane wao ndiyo wamefanya au wamesababisha hayo.

Kwa mfano hivi karibuni mbunge Seleman Zedi ameonekana anakabidhi gari la wagonjwa pale kata ya Itobo, unajiuliza mbunge anahusiana vipi na shughuli hiyo?

Kwamba amenunua yeye gari la wagonjwa kutoka mfukoni mwake au ni pesa ya serikali ambayo ni kodi za wananchi?

Niliwahi kuhoji hili wakati wanatoa taarifa lakini sikujibiwa mpaka leo, nafikiri hawakunijibu kwa sababu wanajua wanadanganya wananchi na hivyo hawataki wajue.

Kwa mantiki hiyo basi, ni wazi kwamba Mbunge wa Bukene ndugu Seleman Zedi ameshindwa kuwatendea haki wananchi wa jimbo la Bukene waliomwamini hapo awali wakati anaomba kwa mara ya kwanza kuwawakilisha wananchi.

Seleman Zedi anajiita "Simba wa vita" lakini haijulikani ni Simba wa vita gani, vita ya kiuchumi au ni vita ya kuwashughulikia watendaji wa chama na serikali ambao wanaonekana kumpinga mambo yake ambayo hayaendani na misingi ya kazi zao?

Katika mazingira hayo, ni ngumu sana kumweka Zedi katika kundi la wanasiasa au kundi la viongozi wa kijamii.

Maana katika sifa za uongozi ni pamoja na uwezo wa kifikra, namaanisha kiongozi anayejishughulisha kufikri kwa sababu ndio kazi kubwa ya Kiongozi.

Kila mtu aliyemzima kiafya anaweza kutenda lakini si kila mtu anaweza kujenga fikra zenye mantiki zinazoweza kuzaa falsafa za kimaendeleo.

Na hii ndiyo sababu Mbunge wa Bukene Seleman Zedi hasikiki kabisa katika medani ya kisiasa.

Nimewahi kwenda mara kadhaa ofisi ndogo ya Makao makuu ya CCM pale Lumumba Dar es Salaam, kilichokuwa kinanishangaza ni kwamba wabunge wa Nzega wanaofahamika ni wawili tu, Dk. Hamis Kigwangalla na Hussein Bashe tu!

Hata alipokuja Mwaandishi wa habari wa ITV hapa Nzega, alifika Bukene kwenye mambo ya kitamaduni (ya asili), wakati anaripoti alitaja eneo la Bukene kama jimbo la Hussein Bashe na sio Seleman Zedi.

Kama ningepata nafasi ya kumshauri Mbunge wa sasa wa Bukene, ndugu Seleman Zedi katika mambo ya kisiasa, ningemshauri aachane na siasa asigombee tena kwa mara nyinyinge, kwa sababu dalili zote zinaonyesha wananchi hawamwitaji kabisa.

Anayepinga hili aende katika jimbo la Bukene na arejee uchaguzi uliopita wa 2020 kuanzia uchaguzi wa ndani ya CCM na ule wa ubunge wenyewe (wa dola).

Ndani ya chama Zedi alitumia nguvu kubwa sana, na upande wa dola CCM kilitumia nguvu kubwa mno, yaani wananchi ni kama walilazimishwa waongozwe na Seleman Zedi.

Tukutane jimbo la Nzega Vijijini....

Kwiyeya Singu. 0784977072

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI