Header Ads Widget

DC CHIKOKA-SERIKALI IMEJIDHATITI KUWAFIKISHIA WANANCHI HUDUMA YA MAJI MJINI NA VIJIJINI

 


Na Shomari Binda-Musoma 

SERIKALI imejidhatiti kuhakikisha inawafikishia wananchi huduma ya maji ya uhakika mjini na vijijini.

Kauli hiyo imetolewa leo machi 21,2025 na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka katika kilele cha Wiki ya Maji 2025 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa manispaa ya Musoma.

Akizungumza na wenyeviti wa mitaa 73 ya manispaa hiyo na wadau mbalimbali wa huduma za maji amesema kwa manispaa ya Musoma zaidi ya asilimia 95 wananchi wamefikiwa na huduma ya maji na kudai hilo ni jambo jema na kuishukuru serikali.


Amesema Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma( MUWASA) imefanya kazi nzuri ya usimamizi wa mradi mkubwa wa maji Bukangc ulioghalimu zaidi ya bilioni 45 zilizopelekea kuwafikishia wananchi huduma.



Chikoka amesema mradi huo licha ya kuwafikishia huduma wananchi wa manispaa ya Musoma lakini pia mradi huo umevifikia baadhi ya vijiji vya Musoma Vijijini na Butiama kutokana na usimamizi mzuri.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan moja ya mkakati ni kumtua mwanamke ndoo kichwani na imepelekea kuwepo kwa miradi mingi ambayo inatekelezwa.

Akisoma taarifa ya MUWASA kaimu mkurugenzi wa mamlaka hiyo Edward Range amesema bei elekezi iliyopitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeshindwa kukidhi gharama ya uendeshaji wa huduma ya maji kwa baadhi ya wananchi mkoani Mara.


Amesema taasisi hiyo inajitegemea kuendesha huduma zake kwa wananchi kwa silimia mia moja kutokana na mapato ya huduma.


"Mapato na gharama ya uendeshaji mheshimiwa mgeni rasmi ni wastani wa shilingi milioni 460 kwa mwezi ukilinganisha na gharama za uendeshaji zenye wastani wa shilingi milioni 615 kwa mwezi sawa na upungufu wa shilingi milioni 155 kwa mwezi "


"MUWASA inatekeleza miradi 6 ambayo ni Manispaa ya Musoma, Mji wa Tarime, Mji wa Mugumu na Musoma DC, ambapo kwa upande wa Manispaa ya Musoma ni mradi wa majitaka kwenye baadhi ya maeneo ya kata za Kitaji, Iringo Mwigobero, Mukendo, Mwisenge na Makoko na mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi 33,657,740,407 ulianza rasmi oktoba 28 mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika aprili 30 mwaka huu 2025",amesema.


Range amesema mamlaka hiyo kwa sasa inatoa huduma ya maji safi kwa wakazi 173,148 sawa na asilimia 98 ya wakazi wa Manispaa ya Musoma, 69,981 sawa na asilimia 52.6 ya watu wanaoishi katika mji wa Tarime, 41,640 sawa na asilimia 70 ya wakazi wa Mji wa Mugumu wilaya ya Serengeti, 21,568 sawa na asilimia 84.5 ya wakazi wa Shitati wilayani Rorya, 47,673 sawa na asilimia 34.1 ya wananchi wanaoishi Musoma DC katika kata za Etaro, Nyegina, Nyakatende na Ifulifu, na 46,873 sawa na asilimia 28.8 ya watu waishio Butiama DC katika kata za Bisumwa, Nyankanga na Bukabwa.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa fedha na Mhasibu wa Mamlaka hiyo Etropia Ndowo amesema kutokana uhaba wa mapato matumizi yanaelekezwa kwenye maeneo ambayo hayana maji na maeneo mengine yaliyo na uhitaji muhimu.


Katika kipindi chote cha Wiki ya Maji kilichoanza machi 17 na kufikia kilele leo machi 21 MUWWSA imekuwa ikitoa elimu na kupokea kero kwenye uwanja wa shule ya msingi Mukendo huku kauli mbiu ya mwaka huu ikisema "Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa Uhakika wa Maji.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI