Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kigoma, Jamal Tamim (kushoto) akikabidhi cheti kwa Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye (kulia) kwa kutambua mchango wake wa usimamizi wa miradi na shughuli za maendeleo mkoani humo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.
Na Fadhili Abdallah, Kigoma.
HALMASHAURI kuu ya CCM mkoa Kigoma imepitisha kwa kauli moja azimio la kumpongeza Raisi Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.
Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma, Jamal Tamim alitangaza azimio hilo la wajumbe wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa Kigoma kilichofanyika Mjini Kigoma ambapo alisema kuwa wajumbe wameridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika kutekeleza miradi ambayo inagusa maisha ya wananchi hivyo wanatoa pongezi kwa utekelezaji huo uliofanyika.
Tamim alisema kuwa wakati wakimpongeza Raisi Samia kwa kazi kubwa aliyofanya katika utekelezaji wa miradi pia wamempongeza Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye na watendaji wa serikali mkoani humo zikiwemo halmashauri za mkoa huo kwa utekelezaji na usimamizi thabiti wa miradi ambao umeleta matokeo chanya katika maisha ya wananchi wa kawaida.
Kwa upande wake Mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM,Abdulkadri Moshi pamoja na kuunga mkono azimio hilo na kuridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika utekeleza wa miradi viongozi wa CCM wa ngazi zote mkoani humo kupitia kamati za siasa za mkoa na wilaya hawana budi kubeba ajenda ya kwenda kwa wananchi kueleza mambo mazuri yaliyofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza miradi ambayo inalengwa kuwakwanua wananchi na kuwaweka hali nzuri ya kiuchumi.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa miradi iliyofanywa mkoani humo Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana mkoa Kigoma umepokea kiasi cha shilingi Bilioni 87.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na kwamba miradi hiyo imeleta matokeo chanya kwenye maisha ya wananchi kiuchumi.
mwisho.
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM Abdulkadri Mushi akizungumza katika mkutano wa halmashauri kuu ya CCM mkoa Kigoma iliyokaa kwa ajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.
Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye akizungumza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi kwa wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM mkoa Kigoma ikiwa ni kueleza taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.
0 Comments