Header Ads Widget

BREAKING:AJALI YA LORI KUGONGA DALADALA MOROGORO

 


Na Matukio Daima Media,Morogoro 

WATU kadhaa wamenusurika Kifo baada ya daladala na lori  kugongana katika eneo la  Kihonda, Manispaa ya Morogoro, kwenye barabara kuu ya Morogoro-Dodoma.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo wakizungumza na Matukio Daima Media eneo la tukio walisema kuwa ajali hiyo ilitokea Alfajiri ya Leo Jumanne Machi 4/2025 .

Kuwa abiria wa daladala hiyo wamejeruhiwa vibaya baada ya daladala hiyo kugongwa kwa nyuma na lori aina ya Fuso. 


"Ajali hii imetokea katika mteremko wa daraja la reli ya Mwendo Kasi (SGR), wakati lori hilo likishuka kwa kasi na dereva wake kushindwa kulimudu, na hatimaye kugonga daladala hiyo iliyokuwa ikipakia abiria kandokando ya barabara"

Mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio wamesema kuwa daladala hiyo ilikuwa imesimama pembeni ili kupakia abiria waliokuwa wakielekea maeneo ya katikati ya mji wa Morogoro, wakati lori hilo likishuka kwa kasi kutoka upande wa Dodoma. 

Dereva wa lori alionekana kupoteza mwelekeo baada ya kushindwa kudhibiti breki, na ndipo gari hilo likatumbukia upande wa kulia wa barabara na kugonga kwa nguvu daladala hiyo iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya kumi na tano.

 Timu ya uokoaji kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wahudumu wa afya walifika haraka katika eneo la tukio na kuanza kutoa msaada wa kwanza kwa majeruhi kabla ya kuwapeleka katika Hospitali .


Wananchi waliokusanyika katika eneo la tukio walionyesha masikitiko yao juu ya ajali hiyo na kuitaka serikali kuweka alama zaidi za barabarani zinazoonyesha tahadhari kwa madereva wanaoshuka kwenye mteremko huo hatari. Walisema kuwa ajali kama hizo zimekuwa zikijirudia mara kwa mara, hasa kutokana na mwendokasi na kutofuata sheria za barabarani.

Kwa upande wao, baadhi ya abiria waliokuwa ndani ya daladala hiyo walisimulia namna walivyopata mshtuko mkubwa baada ya kusikia kishindo kikubwa kabla ya gari yao kugongwa kwa nyuma na kusukumwa mbele kwa umbali wa mita kadhaa. Walisema waliokolewa na abiria wenzao na wapita njia waliokuwa karibu, huku wengine wakipoteza fahamu kutokana na nguvu ya ajali hiyo.

Hadi sasa idadi kamili ya majeruhi pamoja na hali zao inaendelea kufuatiliwa hospitalini, huku polisi wakiendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo mbaya ambayo imesababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa Morogoro na watumiaji wa barabara hiyo kuu ya Morogoro-Dodoma.

Jitihada za kumtafuta Kamanda wa polisi wa polisi wa mkoa wa Morogoro zinaendelea ili kupata undani wa ajali hii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI