Header Ads Widget

TAKUKURU SINGIDA YABAINI KODI YA ZUIO KUTOPELEKWA TRA

 



Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imebaini madudu katika miradi inayotekelezwa katika halmashauri za mkoani hapa ambapo kodi ya zuio imekuwa ikikatwa lakini haiwasirishwi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Sipha Mwanjala, akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2024 alisema tatizo la kukata kodi la zuio na kutowasilisha fedha TRA limejitokeza utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa.


Alisema tatizo limejitokeza katika miradi inayotekelezwa katika Halmashauri ya  Manispaa ya Singida na Halmashauri ya Wilaya ya Singida ambapo mamilioni ya fedha ambazo ni kodi ya zuio yalikatwa lakini hayakupelekwa TRA.


Mwanjala alisema changamoto nyingine waliyoibaini katika utekelezaji wa miradi kwenye halmashauri hizo ni kutozingatia sheria ya ulipaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kodi ya huduma kukatwa lakini haiwasilishwi halmashauri.


Alisema wamebaini pia kukosekana kwa mashine halisi ya EFD kwenye malipo yaliyofanyika kwa mzabuni Cross Bill General Supply and Trading Company Limited aliyekuwa akitekeleza mradi ujenzi wa mabweni,vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Mufumbu iliyopo Manispaa ya Singida kwa thamani ya Sh.milioni 352.2.


Mwanjala alisema baada ya TAKUKURU kufanya uchunguzi katika miradi hiyo na kubaini kasoro hizo fedha zote za kodi ya zuio na kodi ya huduma ambazo zilikatwa lakini hazikupelekwa zilirejeshwa na wahusika na kupelekwa TRA na halmashauri husika.


Aliongeza kuwa katika kipindi hicho TAKUKURU imefanikiwa kuokoa Sh.Milioni 75.369, kati ya hizo Sh.milioni 65.692 ziliokolewa katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwenye mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Mwaja na Mtinko.




Katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Sh.milioni 5.038 ambazo ni makusanyo ya ushuru wa taka ngumu mawakala waliopewa kazi hiyo walizikusanya lakini hawakuziwasilisha halmashauri hivyo baada ya TAKUKURU kufuatilia zilirejeshwa .


Mwanjala alisema katika kipindi hicho cha kuanzia Oktoba hadi Disemba 2024,malalamiko 84 yalipolelewa na kati ya hayo 33 yalihusu vitendo vya rushwa na 51 hayakuhusu vitendo vya rushwa.


Alisema mikakati iliyowekwa na TAKUKURU Mkoa wa Singida katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025 ni kuendelea kufuatilia matumizi ya fedha za serikali zilizoletwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuzuia vitendo vya rushwa katika miradi.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI