Na. Jacob Kasiri - Ruaha.
Bi. Rabia Abdallah mwenye ulemavu wa kusikia kutoka Taasisi ya “Solidarity for Women and Children With Disability” - (SOWOCHIDI) aliyeongazana na watanzania wenzake 56 wenye ulemavu wa aina mbalimbali walikuwa na ziara ya siku mbili ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha kujifunza elimu ya uhifadhi, utalii na kuangalia maeneo mbalimbali yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji.
Wakiwa katika hifadhi hiyo Bi. Rabia alisema, “Tunaiomba serikali kuijumuisha elimu nzuri ya uhifadhi, utalii na jinsi ya kujikinga na wanyamapori wakali katika Mtaala wa elimu kwa Shule za Msingi ili wanafunzi wanapokutana na wanyamapori hao waweze kuepa na kujikinga nao, kwa kufanya hivyo itapunguza madhara yanayopelekea vifo kwa wananchi hususani watoto na wanawake ambao ni waathirika wakubwa.”
Hata hivyo Bi. Rabia hakufurahishwa na vitendo vya ujangili vinavyofanywa na baadhi ya wananchi wanaokaa pembezoni mwa hifadhi hiyo kwa kuendelea kuhujumu rasilimali hizo alisema, “Urithi wetu ni wa thamani sana na ni mali yetu sote, hivyo tushirikiane kuzilinda rasilimali hizi, kwa wale wachache wanaozihujumu sheria iendelee kuwashughulikia ipasavyo.”
Hata hivyo, aliongeza kuwa kupitia kwa mkalimani wa Lugha za Alama wamejengewa uelewa wa masuala ya uhifadhi, utalii na Ujirani Mwema, hivyo waliahidi kuwa mabalozi wa kuwaelimisha wenzao waliobaki kuzifahamu maliasili zetu ambazo taifa la Tanzania limejaliwa kuwanazo na TANAPA imeendelea kuzitunza na kuzihifadhi kwa faida ya sasa na ya Vining’ina vijavyo.
Sanjari na kushuhudia vivutio mbalimbali, waliwashukuru TANAPA kwa kuratibu safari nzima huku wakisema ni nadra sana kwa watu wenye ulemavu kama wao kupata fursa kama hii kutokana na changamoto za gharama za kuingia hifadhini, hivyo waliziomba taasisi nyingine kuiga mfano wa TANAPA ili kuwafadhili na wengine kutembelea vivutio mbalimbali kwa lengo la kujifunza na kuzijua rasilimali zao.
Akiwakaribisha ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa niaba ya Mkuu wa hifadhi hiyo Afisa Uhifadhi Mwandamizi Yasin Sharif anayesimamia Kitengo cha Ujirani Mwema - Ruaha alisema;
“TANAPA itaendelea kushirikiana na Wakalimani wa Lugha za Alama kote nchini ili kutoa elimu ya uhifadhi na utalii kuwafikia watanzania wengi zaidi wenye ulemavu wa kusikia ili kupata elimu itakayochangia kuhamasika kwao na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyomo ndani ya Hifadhi za Taifa hapa nchini.”
Ziara hiyo ya siku mbili ya Watu wenye ulemavu wa kusikia, viungo na ngozi kutoka Taasisi ya “Solidarity for Women and Children With Disability” (SOWOCHIDI) iliyoanza Februari 21, 2025 ilitamatika leo tarehe 23-02-2025 huku watalii hao kutoka Kibaha mkoani Pwani wakifurahia uoto, makundi makubwa ya wanyamapori mbalimbali, ndege na muonekano wa kuvutia wa mto “The Great Ruaha”.
0 Comments