Na. Joyce Ndunguru, Dar es Salaam.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kupitia Pori la AKiba Pande imepanga kuongeza idadi ya wanyamapori takribani 100 kwa ajili ya kuongeza mazao mbalimbali ya utalii katika hifadhi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 4, 2025, Afisa Utalii wa Pori la Akiba Pande, Mustapha Buyogera amesema hadi sasa hifadhi hiyo ina aina mbalimbali za wanyamapori kama vile simba, duma, mamba, pundamilia, nyumbu, pofu, swala pala, swala granti, mbuni, chatu, na White Colobus monkey.
“Hadi sasa Hifadhi ya Pande ina wanyamapori takribani 60 lakini tunakwenda kuongeza wanyama takribani 100 katika hifadhi hii ili kuhakikisha wageni wakifika hapa wanafurahia vivutio vilivyopo ndani ya hifadhi, tunataka kuifanya Pande kuwa kitovu cha utalii katika jiji la Dar es Salaam” amesema Buyogera.
Sambamba na uongezwaji wa spishi mbalimbali za wanyamapori, Buyogera amesema kuwa TAWA imeboresha miundombinu mbalimbali ndani ya hifadhi ili kuhakikisha mtalii akitembelea hifadhi hiyo anapata huduma zote muhimu ikiwemo malazi na sehemu za kupumzika.
Miongoni mwa miundombinu iliyoboreshwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kilometa 10.5, geti la kuingilia hifadhini, sehemu ya kupumzikia wageni (Picnic Site), kambi za Watalii (Camp Sites), njia za utalii (Tourism trail) pamoja na vyoo vya watalii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi, Tawi la Mabwepande James Mbugi alipata wasaa wakutembelea hifadhi ya Pande na amesema kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan inafanya makubwa katika sekta ya utalii na matokeo yanaonekana dhahiri.
“Ilikuwa ni nadra eneo kama Mabwepande kupata hifadhi yenye viwango kama hii kwa sisi tuliozunguka tumeona wanyama wa aina mbalimbali, kuna uwekezaji mkubwa kwelikweli ambao umefanyika hapa” amesema James.
Aidha, ndugu James alitoa rai kwa viongozi vijana na wananchi kwa ujumla kutembelea hifadhi ya Pande kuja kujionea vivutio vya utalii vilivyopo jijini Dar es Salaam.
0 Comments