NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
CHAMA cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Wilaya ya Moshi, mkoa wa Kilimanjaro (Mount Kibo Saccos), kimetoa mkopo wa shilingi milioni 30 kwa wanachama, vikundi, na wanafunzi wa vyuo, lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuinua uchumi wa kila mwananchi.
Mikopo hiyo imetolewa leo kwa wanachama wa vikundi vya Amani Uchao Kusini, kinachojishughulisha na kilimo na ufugaji, na Kikundi cha Yesu Ni Jibu ambapo mikopo hiyo itawawezesha kuongeza ufanisi katika miradi yao na kuboresha maisha yao.
Akizungumza mara baada ya hafla fupi ya kukabidhi mikopo hiyo kwa vikundi viwili shilingi milioni 12, mwanachama mmoja (shilingi milioni 1) na mwanafunzi mmoja (shilingi laki 2), Mwenyekiti wa kamati ya mikopo wa Saccos hiyo, Wilhad Kitali, alisema kuwa wamekuwa wakihimiza na kutoa elimu kwa wananchi wa Wilaya ya Moshi Vijijini na maeneo mengine.
Meneja wa Saccos hiyo, Justine Opola, alieleza kuwa jumla ya mikopo hiyo kwa mwaka huu imetolewa kwa vikundi vitatu vyenye wanachama 60, wanafunzi 15 wa Chuo Kikuu cha Mwenge, pamoja na wanachama tisa.
Alisema kuwa Saccos hiyo imekuwa mkombozi kwa wananchi katika kujitengenezea uchumi imara na kwamba lengo kuu la Saccos hiyo ni kuwa benki ya vikundi, ambapo kwa mwaka ujao wanatarajia kukopesha wananchi kote nchini. Aliongeza kuwa riba ya mikopo hiyo ni nafuu na yenye muda mrefu, ikilenga kuboresha uchumi wa wanachama na wananchi kwa ujumla.
"Mount Kibo Saccos ina miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa ajili ya kuongeza uchumi wa wanachama, ikiwa ni pamoja na mradi wa uchomeleaji, mradi wa matofali, na kutoa huduma za fedha kupitia Wakala," alisema Opola.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo walizungumza kwa nyakati tofauti, akiwemo Frida Kimath kutoka Kikundi cha Yesu Ni Jibu, Kata ya Kibosho Kati, Anna Mushi kutoka Kikundi cha Amani Uchao Kusini, na Christopher Emmanuel, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mwenge, walishukuru Saccos hiyo kwa mikopo ambayo itakwenda kukuza uchumi wao na kuboresha maisha yao.
Chama cha Mount Kibo Saccos kilianzishwa na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Vijijini chini ya Mwenyekiti wake, Cyril Mushi, mwaka 2022. Hadi sasa, chama hicho kina wanachama 185 wanaowekeza hisa zao, akiba na kukopa mikopo yenye riba nafuu. Mikopo hii inawasaidia wanachama kujikwamua kiuchumi ikilinganishwa na mikopo mingine.
Mwisho.
0 Comments