Na Matukio Daima media
MTAALAM wa uwekezaji ambae ni Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Ukumbi, wilaya ya Kilolo, Festo Kipate, ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi yake ya kujenga barabara ya lami kutoka Iringa hadi Kilolo.
Kwa mujibu wa Kipate, barabara hiyo sio tu kwamba itarahisisha usafiri kwa wananchi, bali pia itakuwa chachu ya maendeleo kwa wakulima wa wilaya hiyo, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya miundombinu duni.
Akizungumza katika kipindi cha Tanzania ya Leo kinachorushwa na Matukio Daima TV, Kipate alisema kuwa kwa miaka mingi, wananchi wa Kilolo wamekuwa wakihangaika kusafirisha mazao yao kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Kuwa hali hiyo ilipelekea kupungua kwa faida ya wakulima kwani usafirishaji wa mazao ulikuwa mgumu, mazao kuharibika kabla ya kufika sokoni, na gharama za usafirishaji kuwa juu.
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukilia kuhusu barabara hii, lakini sasa tunashukuru kuwa serikali ya Rais Samia imekuwa sikivu na imetekeleza ahadi yake kwa vitendo.
Alisema ujenzi wa barabara hii ya lami ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Kilolo, hasa wakulima ambao sasa wataweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kuuza kwa bei nzuri," alisema Kipate.
Kuwa Kilolo ni mojawapo ya wilaya zinazotegemea sana kilimo kama nguzo kuu ya uchumi mazao kama mahindi, viazi, mbogamboga, matunda, chai, na mazao mengine huzalishwa kwa wingi katika wilaya hiyo.
Hata hivyo, kwa miaka mingi, wakulima wa Kilolo wamekuwa wakipata changamoto kubwa ya kusafirisha mazao yao kwenda kwenye masoko ya Iringa Mjini, Morogoro, Dodoma na hata Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kipate, changamoto kubwa imekuwa ni ubovu wa barabara, hasa wakati wa mvua ambapo magari hushindwa kupita, na hata wale wanaoweza kusafirisha mazao hulazimika kutumia gharama kubwa kwa usafiri.
Kuwa kero hiyo ilikuwa inaathiri pato la wakulima kwani mazao mengi huishia kuoza kwa kukosa soko la haraka.
"Tunajua kuwa uchumi wa Kilolo unategemea sana kilimo, lakini bila barabara nzuri, juhudi za wakulima zinaweza zisizae matunda hata wawekezaji wanapokuja kuwekeza kwenye kilimo au viwanda vya kuchakata mazao wanahitaji uhakika wa miundombinu bora ili waweze kusafirisha bidhaa kwa urahisi. Kwa hiyo, kujengwa kwa barabara hii ya lami ni hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa wilaya yetu," alisema Kipate.
Kipate alieleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Kilolo kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuboresha Usafiri na Usafirishaji – Barabara ya lami itapunguza muda wa safari kati ya Iringa na Kilolo, hivyo kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.
Kwani Wakulima wataweza kusafirisha mazao yao kwa haraka na kupunguza upotevu wa mazao shambani ,kuimarisha Uchumi wa Kilimo – Kwa kuwa Kilolo ni eneo la kilimo, barabara hii itaongeza thamani ya mazao kwa kuhakikisha yanawafikia walaji kwa muda mfupi, hivyo kuongeza kipato cha wakulima.
Pamoja na kuvutia Wawekezaji kwani Miundombinu bora huwahamasisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo ya uzalishaji na usindikaji wa mazao ,Barabara ya lami itachochea uwekezaji wa viwanda vidogo vya kuchakata kahawa, chai, na matunda, jambo ambalo litasaidia kuongeza ajira kwa wananchi wa Kilolo.
Alisema kuwa barabara hiyo itapunguza Gharama za Usafiri – Ubovu wa barabara huongeza gharama za usafirishaji wa bidhaa, lakini kwa kuwa barabara itakuwa ya lami, gharama hizo zitapungua, na kufanya bidhaa ziwe nafuu kwa walaji kuwa Usafiri rahisi utaongeza upatikanaji wa huduma muhimu kama afya na elimu kwa wananchi wa Kilolo. Wagonjwa wataweza kufika hospitali kwa haraka, na wanafunzi watapata nafasi ya kusafiri kwenda shule bila kikwazo cha barabara mbovu.
Kipate alisema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kufanya jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara kote nchini ili kuwezesha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kuwa mkoa wa Iringa, ikiwa ni moja ya mikoa inayojulikana kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo, umepewa kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu bora.
Kipate alibainisha kuwa wananchi wa Kilolo wana matumaini makubwa kuwa barabara hiyo itakamilika kwa wakati na kuleta mabadiliko makubwa katika maisha yao.
"Tunatoa shukrani kwa serikali kwa kutimiza ahadi yake, na tunatarajia kuona maendeleo makubwa kupitia barabara hii. Wananchi wa Kilolo wako tayari kuchangamkia fursa hii na kutumia barabara hii kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii," alisema Kipate.
Barabara ya lami kutoka Iringa hadi Kilolo ni moja ya miradi muhimu ya miundombinu inayotarajiwa kuleta maendeleo makubwa kwa wakulima na wananchi wa Kilolo kwa ujumla.
Kujengwa kwa barabara hii kutarahisisha usafirishaji wa mazao, kuvutia uwekezaji, na kuinua hali ya maisha ya wakazi wa Kilolo.
Serikali ya awamu ya sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, na barabara hii ni moja ya mifano hai ya utekelezaji wa ahadi kwa vitendo.
Kipate ambae kitaaluma ni mtaalam wa fedha na uwekezaji mwenye Master ya Sayansi na uwekezaji ya chuo Cha Coventry London alisema Kuwa Wakulima na wananchi wa Kilolo sasa wana matumaini mapya ya kujikwamua kiuchumi kupitia barabara hii ya lami, ambayo itabadilisha kabisa taswira ya maendeleo ya wilaya hiyo.
0 Comments