Header Ads Widget

MKANDARASI WA JENGO LA UTAWALA ILEJE AONYWA.

 


 

Na Moses Ng'wat, Ileje.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, kuunda kamati maalum itakayojumuisha vyombo vya usalama ili kuchunguza mwenendo wa ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika  kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo, ambapo hadi sasa umefikia asilimia 30 pekee, huku siku 287 kati ya 450 zilizotengwa kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo zikiwa zimepita.

Chongolo ametoa agizo hilo, Februari 12, 2025, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo na kubaini ucheleweshaji wa utekelezaji wake, licha ya serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 593.7 kati ya shilingi bilioni 2 zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameipa kampuni inayojenga jengo hilo, Mbuya Contractors Co. Ltd & JV Chiganda Contraction Co. Ltd, muda wa mwezi mmoja kuhakikisha inarejesha kasi ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia ratiba ya kazi.

Ameonya kuwa endapo mkandarasi huyo atashindwa kutekeleza agizo hilo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, ikiwemo kuifikisha kampuni hiyo katika Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kwa ajili ya hatua zaidi.




Kwa mujibu wa taarifa ya ujenzi, kiasi cha shilingi milioni 593.7 kimetumika hadi sasa kati ya shilingi bilioni 2 zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo.

Akizungumzia changamoto za ucheleweshaji wa mradi huo, Mhandisi Samweli Mkuki, kwa niaba ya mkandarasi, alisema kuwa ucheleweshaji huo ulitokana na matatizo ya kifedha, lakini kwa sasa wameanza kuchukua hatua za kurejesha kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, alieleza kuwa kuna wasiwasi mkubwa kuhusu kukamilika kwa wakati kwa jengo hilo kutokana na mkandarasi kushindwa kufuata masharti ya mkataba.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI