Na Fadhili Abdallah,Kigoma
IMEELEZWA kuwa mashamba yasiyoendelezwa yamekua chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi wilayani Kakonko mkoani Kigoma ikiwemo mashamba ya kurithi ambayo hayana nyaraka zozote za umiliki.
Afisa ardhi wa halmashauri ya wilaya Kakonko, Gideon Kimaro alisema hayo wakati wa muendelezo wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea na mikutano mbalimbali ya wananchi wilayani humo ambapo alisema kuwa wananchi kuchukua maeneo kwa ajili ya kilimo na makazi imekuwa chachu ya kuongezeka kwa migogoro ya ardhi wilayani humo.
Akieleza kuhusu hilo afisa ardhi huyo wa Halmashauri ya wilaya Kakonko amesema kuwa serikali kupitia serikali za vijiji imekuwa ikiweka mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuwezesha kuondokana na migogoro inayoweza kujitokeza ili kila shughuli ifanyike maeneo yaliyoanishwa na wananchi wanapaswa kutumia ardhi hiyo kulingana na mipango iliyowekwa.
Akizungumza katika mikutano hiyo Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya Kakonko, Nicholous Muhebera alisema kuwa migogoro mingi vijijini inasababishwa na1 ukiukwaji wa sheria za ardhi namba nne na namba tano za1 mwaka 1999 ambazo zinataka wanaotaka kumiliki ardhi kufuata sheria hizo na1 kwamba hiyo ndiyo njia pekee ambayo itamuwezesha mwananchi kumiliki ardhi1 kihalali na kutoingia kwenye mgogoro na serikali au na1 mwananchi mwenzake.
Kwa upande wake mratibu wa kampeni za msaada wa kisheria wa Mama Samia, Jackline Kulwa alisema kuwa katika kampeni hiyo ya siku 10 wilayaani Kakonko wanatarajia kufika kwenye kata 10 na kuvifikia vijiji 30 ambapo watatoa msaada wa kisheria, miongozo na kusikiliza kero za wananchi ili ziweze kufanyiwa kazi kulingana na sheria na taratibu za nchi.
Kulwa alisema kuwa kampeni hiyo imefika hadi vijijini vya mbali kabisa mbali na makao makuu ya wilaya au kata ili kuwezesha kusikilizwa kwa kero za wananchi zilizosababisha kukosa haki zao mbalimbali hivyo wote watakaojitokeza kesi zao zitasikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi kwenye mamlaka zinazohusika na malalamiko yaliyotolewa.
Mwisho
0 Comments