Na Lilian Kasenene, Morogoro, Matukio DaimaApp
KUTOKANA na kuwepo kwa changamoto ya miundombinu ya Barabara isiyo ya kuridhisha ndani ya Manispaa ya Morogoro, imeifanya Halmashauri hiyo ya Manispaa kununua mtambo wa kuchonga barabara(Grader)la thamani ya shil.Bil.1.3.
Mtambo huo utaboresha Barabara kwa kiwango cha changarawe zilizopo katika mitaa 295 kwenye kata 29 za Manispaa ya Morogoro.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,Emanuel Mkongo akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mtambo huo baada ya kukamilisha kikao cha baraza la madiwani cha kawaida katika robo ya pili ya mwaka 2024/2025,alisema uwepo wa mtambo huo utakuwa mkombozi kwa wananchi baada ya barabara hizo kuchongwa.
Mkongo alisema kuwa mtambo huo umenunuliwa baada ya baraza
la madiwani kuazimia kutokana na kuwepo kwa changamoto ya miundombinu siyo ya kuridhisha zinaunganisha kwenye mitaa na maeneo yanayotolea huduma.
“Kwa baada ya kununua mtambo huu hatua inayofuata ni kukamilisha taratibu nyingine za kisheria ikiwemo vikao vya kamati maalum ya wataalamu na madiwani kuweka utaratibu wa matumizi ya mtambo huo ili uweze kutumiwa kwenye mitaa na kata zenye changamoto za miundombinu.”alisema Mkongo
Aidha,alisema kuwa mtambo huo pia utakodiwa katika maeneo ambayo hawana huduma hiyo ikiwa ni sehemu ya kutoa huduma kwa kuchangia gharama za uendeshaji kwa masilahi mapana kwa umma.
Meya wa Manispaa ya Morogoro,Paschal Kihanga alisema ya kuwa halmashauri ya Manispaa ya Morogoro katika mipango yake ni kuhakikisha ya kuwa barabara zote zilizopo katika Manispaa hiyo zitafanyiwa matengenezo kwa kushirikiana na TARURA.
Kihanga alisema kuwa kutokana na ushirikiano kati ya madiwani wa halmashauri hiyo na wataalamu wake wamepata mafanikio makubwa na kufanikiwa kununua mtambo wa kuchoronga barabara ikiwa ni mkakati wa kuufanya mji wa Morogoro kuwa Jiji.
Diwani viti maalum,Manispaa ya Morogoro Latifa Ganzel,alishukuru ofisi ya mkurugenzi kwa kufanyia kazi maazimio ya madiwani kwa vitendo kwa kununua mtambo huo wa kuboresha miundombinu ya barabara.
Latifa alisema kwa kipindi kirefu Halmashauri hiyo ya Manispaa ilikuwa na changamoto ya kupata mtambo wake jambo lililokuwa likighalimu kukodi mtambo kwa ajili ya marekebisho ya barabara.
Alisema kuwa tangu uamuzi wa madiwani wa halmashauri kuazimia uwepo wa manunuzi wa mtambo wa kuchonga miundombinu ya barabara,ofisi ya mkurugenzi imechukua hatua ya haraka katika kukamilisha mchakato wa manunuzi na hatimae kupatikana na mtambo huo,ambao kwa sasa umekuwa ni mwarobaini ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
Katika hatua nyingine,Mwenyekiti wa CCM,Wilaya ya Morogoro Mjijini Fikiri Juma alishauri uongozi wa Manispaa hiyo wakati wakiendelea na mchakato wa namna bora katika matumizi ya mtambo huo,wajikite zaidi katika kuboresha barabara zinazotoa huduma kama shule, zahanati,Vituo vya afya na Hospitali ili kuharakisha huduma hizo ziwafikie wananchi kwa haraka.
Juma alisema hali ya miundombinu ya barabara katika manispaa ya Morogoro ilikuwa si ya kuridhisha lakini baada ya kupatikana kwa mtambo huo,changamoto ya miundombinu ya barabara itakuwa ni historia.
0 Comments