Header Ads Widget

VIKUNDI 467 VYA WANAWAKE, VIJANA NA WENYE ULEMAVU MOROGORO KUPATIWA SH BIL 11.5


Na Lilian Kasenene,Morogoro

KIASI Cha Sh Bil 11.5  zimeidhinishwa na Serikali na zinatarajiwa kutolewa kwa vikundi 467 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu vilivyokidhi vigezo vya kupata mkopo wa asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya  Halmashauri.

Afisa Maendeleo ya jamii mkoa wa Morogoro Dickson Makoba alisema  hayo jana wakati akitoa taarifa  ya hali ya utoaji mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10.

Makoba alisema hadi kufikia Desemba 31 mwaka 2024 halmashauri zote za mkoa wa Morogoro zimekamilisha awamu ya kwanza ya taratibu za utoaji mkopo kwa vikundi  vya wanawake(293), vijana(147) na watu wenye ulemavu(38).

"Watu wenye ulemavu tu watapatiwa kiasi cha shilingi milioni 849.1,"alisema.

Afisa huyo alisema kuanzia mwezi Aprili 2023  Serikali ilisitisha utoaji mikopo inayotokana na  asilimia kumi  mapato ya ndani ya halmashauri ili kutengeneza utaratibu mzuri utakaowezesha wanufaika  kukopa na kurejesha kwa wakati.

Alisema ili kuondokana na changamoto  ya vikundi kutorejesha mikopo wanayopewa na Serikali  imefanya mabadiliko katika kanuni na muongozo wa utoaji mikopo kwa vikundi hivyo.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro  Adam Malima alisisitiza kutokuwa na urasimu katika utoaji mikopo hiyo ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo hiyo.

Pia alisisitiza  kuwa fedha hizo kwa sasa zitakuwa na usimamizi na ufuatiliaji wa hali ya juu kutokana na matumizi mabaya ya vikundi hewa  yaliotokea hapo awali .

"Wapo watu walitengeneza vikundi hewa wakachukua fedha na kisha mikopo haikulipwa, ndipo Rais  Samia Hassan Suluhu akasitisha kwa muda" alisema.

Naye katibu tawala mkoa wa Morogoro Dk Mussa Ali Mussa akazitaka halmashauri za wilaya kuunga mkono vikundi vinavyopewa mikopo kwa kununua bidhaa zao.

"Halmashauri ziwaelimishe wenye vikundi vinavyoomba mikopo viwe vinazalisha, vikundi vingi havizalishi ndio maana vibashindwa kurejesha mikopo" alisema.

Mwenyekiti wa Chama Cha Ualibino(TAS)Morogoro Hassan Mkazi alisema ipo changamoto ya watu wenye ulemavu kutokana  mfumo wa kieletroniki ya kuomba mkopo hususani kwa wenye uoni hafifu, wasiosikia na wasioona .


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI