Na Fadhili Abdallah,Kigoma
POLISI mkoani Kigoma imemtia mbaroni mtu mmoja mkazi wa kijiji cha Nyakayaga wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma akiwa na ngozi za Chui na nyara mbalimbali za serikali bila kuwa nyaraka zinazomruhusu kumiliki vituo hivyo.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma kuhusu operesheni mbalimbalizi zilizofanywa na jeshi hilo alisema mtuhumiwa ambaye jina lake limehifadhiwa alikamatwa na polisi mwwishoni mwa wiki iliyopita kijijini hapo.
Pamoja na vipande viwili vya ngozi ya Chui kamanda Makungu alisema kuwa mtuhumiwa alikamatwa pia na ngozi ya ndege aina ya Mwewe na pembe moja ya Mnyama anayejulikana kama Insha ambapo upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani.
Katika tukio lingine polisi mkoani Kigoma imewatia mbaroni watu wanne wakazi wa maeneo ya Kata ya Buzebazeba Manispaa ya Kigoma Ujiji wakiwa na pikipiki mbili ambazo zinaaminika kuwa ziliibwa kwa wamiliki halali.
Alizitaja pikipiki hizo ni aina ya TVS iliyokua ikitumia namba bandia ya usajili MC 510 DHP wakati namba yake halisi ni MC 971 CPV na MC 510 DHP ambayo ilikuwa na namba bandia za usajili MC 448 BQQ ambapo moja
iliibwa kwenye soko la jioni maarufu Soko Marungu manispaa ya Kigoma Ujiji na pikipiki nyingine iliibwa katika baa inayojulikana kwa jina la The Breeze iliyopo mjini Kigoma.
Mwisho.
0 Comments