Na Thobias Mwanakatwe, ITIGI
BOHARI ya Dawa (MSD) imetoa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh.Milioni 210 katika Hospitali ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida ambayo inatarajia kuzinduliwa na kuanza kutoa huduma za matibabu rasmi kwa wananchi Februari 2025.
Meneja wa MSD Kanda ya Kati, Mwanashehe Jumaa, amekabidhi vifaa hivyo juzi kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dk.Vicent Mashinji, katika hafla iliyofanyika hospitalini hapo na kuhudhuriwa na wananchi.
Jumaa alitaja baadhi ya vifaa vilivyotolewa kwa hospitali hiyo kuwa ni mashine ya usingizi,vitanda kwa ajili ya kujifungulia wajawazito,taa za kufanyia operesheni,mashine ya kufanyia usafi na friji ya damu.
Vingine ni mashine za kupima uzito kwa watoto wanaozaliwa ambayo ina uwezo wa kumpima mtoto uzito na urefu,mashine ya kusaidia wagonjwa kupata hewa tiba,meza na mashine ya kufulia nguo.
Meneja huyo alisema vifaa hivyo vilivyotolewa ni baadhi tu kati ya vifaa vya Sh.Milioni 300 ambavyo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi ilitoa maombi na kwamba vilivyobaki vitaletwa ili lengo tarajiwa la kuimarisha huduma za afya linafikiwa na kuhakikisha uzazi unakuwa salama.
"Tunamshukru mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kununulia vifaa hivi ambavyo vitasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi," alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Manyoni,Dk.Mashinji, alimshukru Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha maendeleo yanakwenda kwa wananchi ambapo sekta ya afya katika wilaya hiyo hakuna mwananchi anayetembea umbali wa kilometa tatu kufuata huduma za matibabu.
"Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alishawahi kusema ukiwa na maendeleo ya vitu bila maendeleo ya watu hayo maendeleo hayana maana,kwa hiyo rais wetu (Dk.Samia) anatekeleza kwa vitendo maendeleo ya vitu yanakwenda sambamba na maendeleo ya watu," alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi,Ayoub Kambi, alisema vifaa hivyo vilivyotolewa na MSD vitasaidia kuondoa changamoto kwa wananchi katika kupata huduma za matibabu hospitali hiyo itakapoanza kutoa huduma rasmi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Hassan Simba, alisema hospitali hiyo ambayo itaanza kutoa huduma Februari mwaka huu hadi sasa zimeshatumika Sh.Bilioni 1.750 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba na kwamba watumishi 42 watakaoanza kutoa huduma tayari wameshaletwa.
"Tunamshukru rais Dk.Samia kwa kutupatia fedha za ujenzi wa hospitali hii pamoja na za kununulia vifaa tiba hakika hakika huduma bora zitakuwa zinatolewa na wananchi kuzifurahia," alisema.










0 Comments