Na Matukio Daima Media
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC), Salim Abri Asas, anatarajiwa kuwaongoza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa katika uzinduzi wa maadhimisho ya Sherehe za Miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama hicho.
Sherehe hizo zitafanyika kesho Jumanne Januari 28, 2025, katika kata ya Ng’uruwe, wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilolo, John Kiteve, maandalizi ya uzinduzi huo yamekamilika kwa asilimia kubwa.
Alieleza kuwa kufanyika kwa sherehe hizo katika kata ya Ng’uruwe ni mkakati wa chama kuhakikisha kinaendelea kufikia wanachama wa maeneo ya vijijini na kuwaunganisha katika shughuli za maendeleo ya chama.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Miaka 48 ya CCM: Shiriki Uchaguzi kwa Uadilifu na Kazi Iendelee”.
Kauli mbiu hii inalenga kuwahamasisha wanachama kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, huku wakiunga mkono juhudi za maendeleo zinazoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kiteve alisema kuwa tofauti na vyama vya upinzani ambavyo hufanya shughuli zao mijini, CCM imeendelea kuwa chama cha watu wote, bila kujali eneo.
“Tuliona ni muhimu sherehe hizi zifanyike hapa Ng’uruwe, ili wananchi wa maeneo haya nao wahisi sehemu ya chama na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya muhimu,” alisema.
Aidha, Kiteve aliongeza kuwa uzinduzi wa sherehe hizo ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho makubwa ya kuzaliwa kwa CCM, ambayo hufanyika Februari 2 kila mwaka.
Katika wilaya ya Kilolo, sherehe hizo zitatanguliwa na shughuli mbalimbali za kichama na maendeleo katika kipindi chote cha maandalizi.
Akizungumza kuhusu mgeni rasmi wa uzinduzi huo, MNEC Salim Abri Asas, Kiteve alisema kuwa amekuwa nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya CCM katika wilaya ya Kilolo na mkoa wa Iringa kwa ujumla.
“Asas amechangia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha chama kinaendelea kuwa na uhai.
Amefadhili ujenzi wa ofisi za chama, kusaidia mikutano ya kichama, na hata kusaidia ushindi wa CCM katika chaguzi mbalimbali,” alisema.
MNEC Asas pia amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo katika chaguzi za serikali za mitaa, vitongoji, na vijiji.
Kiteve aliongeza kuwa msaada huo unawapa wanachama wa CCM wilaya ya Kilolo hamasa kubwa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ambao Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, akiwa na mgombea mwenza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Wanachama wa CCM katika wilaya ya Kilolo wameonesha shauku kubwa ya kushiriki katika maadhimisho haya, ambayo yanatarajiwa kuwa ya kihistoria.
Kiteve alisisitiza kuwa maandalizi yote yamekamilika, na wanachama wanakaribishwa kushiriki kikamilifu ili kusherehekea mafanikio ya chama chao.
Sherehe hizi ni fursa muhimu kwa wanachama wa CCM kuonesha mshikamano na kuimarisha umoja ndani ya chama, huku wakiendelea kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
USIKOSE KUFUATILIA MUBASHARA TUKIO HILI MATUKIO DAIMA TV
0 Comments