Na Moses Ng'wat, Tunduma
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba, mkoani Songwe, limeeleza wasiwasi wake kuhusu kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa kipande cha barabara ya mchepuo kutoka Mwakabwangazi hadi
Transfoma chenye urefu wa kilomita 10.
Madiwani wamesema kuwa, barabara hiyo ni muhimu katika kupunguza msongamano wa magari, hususan malori, kwenye barabara kuu ya Tanzania -Zambia (Tanzam), ikiwemo ajali zinazogharimu maisha ya wananchi.
Diwani wa viti maalumu, Tusalighwe Mwotela, akiuliza swali katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwenye kikao cha kupitia taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25, alitaka kujua lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza na kukamilika ili kupunguza adha ya foleni kwa wananchi.
Akijibu swali hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Innocent Maduhu, alisema kuwa bajeti ya mradi huo imeshatengwa na hatua ya manunuzi inaendelea, huku akisisitiza kuwa ujenzi utaanza mara fedha kutoka Serikali Kuu zitakapopatikana.
Kwa upande wake, akitoa majibu ya nyongeza, Mwenyekiti wa Halmashauri, Ayubu Mlimba, aliwataka alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa fedha kutoka serikali kuu na kwamba pindi fedha zitakapoletwa utaanza utekelezaji wake.
Aidha, Mwenyekiti Mlimba amewataka madiwani kushirikiana katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, huku akatoa wito kwa Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine zinazohusika kudhibiti magari yenye uzito mkubwa kupita kiasi kuingia kwenye barabara za ndani za mji huo ili kuzuia uharibifu na kuzilinda barabara hizo.
Katika kuweka mikakati ya kudumu dhidi ya foleni na msongamano, tayari serikali imepanga kuanza ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa (Mbeya) hadi Tunduma (Songwe) yenye urefu wa kilomita 218, kwa gharama ya shilingi trilioni 1.33 kama mkakati mwingine wa kupunguza foleni kwa malori ya mizigo kutoka bandari ya Dar es salaam kwenda katika mpaka wa kwenda nchi za kusini mwa Afrika.
0 Comments