Header Ads Widget

WAKULIMA WA PARETO ILEJE WAPATIWA KILO 400 ZA MBEGU BORA KUTOKA TARI UYOLE.

 


Na Moses Ng'wat, Songwe.

WAKULIMA 1,600 kutoka kata nne za Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Mkoani Songwe, wamepatiwa kilo 400 za mbegu bora za Pareto kwa ajili ya uzalishaji wenye tija kutoka katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Tawi la Uyole.

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi mbegu hizo, zilizopokelewa leo Disemba 13, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi aliyeambatana na wakulima wachache, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amesema upatikanaji wa mbegu hizo ni jitihada za serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini.


Chongolo amesema mbegu hizo za Pareto kiasi cha kilo 400 zilizozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Tawi la Uyole zinaenda kuongeza ekari mpya zaidi ya 1,000 za uzalishaji wa zao hilo Mkoani humo na kuchangia ongezeko la wastani wa takriban tani 720 za maua makavu kwa mwaka.


"Nimeambiwa na watafiti kuwa mbegu hizi zina tija kubwa na zina uwezo wa kuzaa maua makavu kati ya kilo 450 hadi 500 kwa ekari na kiwango cha ubora wa kiuatilifu (Sumu) kinachopatikana ni kati ya asilimia 1.8 hadi asilimia 2". Amefafanua zaidi Chongolo


Katibu Tawala mkoa wa Songwe Hapines Seneda

Aidha, Chongolo ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali na kusema katika mwaka wa fedha wa

2024/2025, imetenga bajeti ya kiasi cha Shilingi milioni 197 kwa ajili ya utafiti na uzalishaji mbegu za pareto kupitia kituo cha Utafiti cha TARI Uyole.


"Kitendo hiki ni cha kupongezwa kwa kuwa zaidi ya miaka 30 hakuna fedha iliyowahi kutolewa na Serikali kwa ajili ya kusaidia kuzalisha mbegu bora za pareto nchini,  isipokuwa kwa awamu hii ya sita (6) ya Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan na tunapaswa kumpongeza sana Rais kwa hatua yake hiyo ya kujali wakulima wa zao la pareto" alisema Chongolo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchnganyiko (COPRA), Irene Mlola, amesema 

 uzalishaji wa zao la Pareto umeendelea nchini kutoka tani 3500 hadi tani 4000 na kuifanya Tanzania kuwa ya pili duniani kwa uzalishaji wa zao hilo, ikitanguliwa na nchi ya Tasmania.

Pia amesema fedha za malipo ya wakulima yamekuwa yakiongezeka kutoka shilingi Bilioni 6.2 katika  msimu wa kilimo wa 2020/21 na kufikia shilingi Bilioni 14.8 kwa msimu wa mwaka wa 2022/ 2023, huku mauzo ya nje ya nchi yakiongezeka kutoka shilingi Bilioni 15 hadi shilingi Bilioni 24.1.


"Bei elekezi ya serikali katika msimu uliopita ilikuwa shilingi 3,500 kwa kilo na msimu huu bei elekezi tuliyoitangaza kama mwezi mmoja uliopita inatarajiwa kuwa shilingi 5,000 kwa kilo" alisema Mlola.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mgomi ameipongeza serikali kwa juhudi mbalimbali za kuwainua wakulima hasa kuwapatia kiasi hicho cha kilo 400 mbegu za Pareto ambazo amesema zinaenda kuongeza tija kubwa na kuimarisha uchumi wa  wakulima wa Wilaya hiyo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI