Na Fadhili Abdallah,Kigoma
VIKAO vya ujirani mwema baina ya Tanzania na Burundi vilivyoanzishwa miaka 20 iliyopita vinaelezwa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiusalama baina ya nchi hizo na vikao hivyo vimesaidia kutatua changamoto nyingi zilizokuwa zikijitokeza katika Nyanja hizo.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Mstaafu, Elmon Mahawa alisema hayo katika kikao cha ujirani mwema baina ya nchi hizo kilichofanyika mjini Kigoma jana kikiwa maalum kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa vikao hivyo.
Mahawa ambaye alikuwa Mkuu wa mkoa Kigoma kuanzia mwaka 2003 hadi 2006 alisema kuwa kuanzishwa kwa vikao hivyo kunatokana na mkoa Kigoma kukabiliwa na changamoto kubwa ya kiusalama ambayo ilisababishwa na wimbi kubwa la Wakimbizi kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo hivyo kuanzishwa kwa vikao hivyo kulikuwa na lengo la kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikijitokeza.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Mstaafu wa Makamba nchini Burundi, Kanali Mstaafu Reverien Ndikuriyo ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Chama Tawala Nchini Burundi cha CNDD – FDD alisema kuwa wakati wanaanza vikao hivi kulikuwa na kutupiana lawama hasa changamoto za usalama zilizoanzishwa na wakimbizi ambazo vikao vilijadili na kuzipatia ufumbuzi.
Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa wananchi wa mkoa Kigoma na mikoa ya Burundi inayopaka na mkoa Kigoma wanafanana kwa mambo mengi hivyo vikao hivyo vya ujirani mwema vinayo nafasi kubwa ya kuendelea kuchakata na kujadili masuala ya ulinzi na usalama, uchumi na biashara, michezo na masuala ya utamaduni.
0 Comments