Header Ads Widget

SHILINGI BIL 2.9 KUKARABATI CHUO CHA UTABIBU MASWA


Na Matukio Daima App, Maswa.

NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetangaza kutoa kiasi cha shilingi Bil. 2.9 kwa ajili ya kujenga upya Chuo cha Maafisa Tabibu kilichopo wilayani Maswa Mkoani Simiyu.

Amesema Uamuzi huo umetokana na Uchakavu wa majengo ya chuo hicho, ambacho kimekuwa kikitoa huduma kwa zaidi ya miaka 50 na kwamba hali ya dharura inahitajika ili kuboresha miundombinu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia.


Naibu Waziri wa Afya, ameyasema hayo juzi wakati wa mahafali ya 48 ya chuo hicho yaliyofanyika mjini Maswa, alipokuwa mgeni rasmi huku alieleza kuwa chuo hicho kimechangia kuzalisha Maafisa Tabibu wanatoa huduma muhimu za afya nchini.

Alisema Chuo hicho kitaimarishwa kwa ujenzi wa miundombinu ya majengo na vifaa vya kujifunzia vya kisasa, Kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mafunzo bora zaidi na vifaa vya kisasa, hatua itakayosaidia kuongeza ubora wa huduma za afya kwa Watanzania.

"Hatua hii inaonyesha dhamira ya serikali kuboresha sekta ya afya kupitia uwekezaji katika elimu ya afya na kuimarisha uwezo wa vyuo vya kitaaluma kutoa mafunzo ya kiwango cha juu...Ni maendeleo makubwa yanayotarajiwa kuleta mabadiliko chanya kwa sekta ya afya nchini" amesema na kuongeza.

“Niwape tu taarifa Rais wenu, ninyi mnaomaliza.. mje mtembelee chuo chenu mwakani mwezi wa sita mtatakuta chuo kipya, utatamani urudie shule nataka kuwahakikishia Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan ametoa Sh Bilioni 2.9 kwa ujenzi wa chuo hiki”.

Amesema kuwa chuo hicho ambacho kilianzishwa mwaka 1974 kilianza kutoa kozi ya  cheti kwa Waganga Wasaidizi Vijijini na sasa kinatoa Stashahada ya Utabibu na ni miongoni mwa vyuo nchini ambavyo wahitimu wake wamekuwa wakifanya vizuri wanapokwenda kutoa huduma kwa wananchi.


Awali Rais wa serikali ya Wananchuo wa chuo hicho,.Simba Gulala amesema kuwa katika kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho na kufanyika kwa mahafali ya 48 lakini bado kuna changamoto ya  uchakavu  na upungufu wa majengo yakiwemo  Madarasa, Hosteli, Bwalo, Maabara pamoja na vifaa vya kufanyia mazoezi na hivyo kuwafanya kusoma katika mazingira yasiyo rafiki.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Hangwa Enos Hangwa amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Maafisa Tabibu Maswa hadi sasa kimeweza kuandaa wataalam 2,255 katika fani ya Utabibu na kina miliki eneo lenye ukubwa wa hekta 6.11 hivyo lina nafasi kubwa ya uendelezaji wa miundo mbinu ya majengo.

Amesema kuwa kwa sasa chuo hicho kinatoa fani moja pekee ya stashahada ya Utabibu huku kikiwa na vyumba viwili vya madarasa,maabara ya tiba moja,bwalo moja,jengo la utawala lenye ofisi nane ,jiko moja na mabweni 14 yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 112 pamoja na nyumba nne za watumishi ambapo majengo yote yanahitaji ukarabati mkubwa.

 


Agape Slivester mkazi wa Chato mkoani Geita ambaye ni miongoni mwa wazazi waliofika kushuhudia mahafali hayo amesema kuwa uamuzi wa  Serikali kuamua kujenga upya chuo hicho  inaashiria dhamira yake kuimarisha elimu ya afya na kuboresha miundombinu ya kufundishia.

 

“Uwekezaji huu utasaidia kuongeza idadi ya maafisa tabibu, kuboresha mazingira ya kusomea na kufundishia na hatimaye kuboresha huduma za afya kwa Watanzania,” amesema.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ameeleza kuwa kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani wilaya hiyo ilikuwa na vituo vya afya vutatu lakini kwa sasa vipo sita na wilaya hiyo imepokea fedha nyingi kutoka serikalini  zaidi ya Shilingi Bilioni 70 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ya sekta ya afya.

“Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Maswa nimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoifanya ya kuiletea maendeleo wilaya yetu kwa kipindi cha miaka minne sasa tangu aingie madarakani,wilaya hiyo imeshapokea zaidi ya Sh Bilioni 70 kwa ajili ya miundo mbinu ya miradi mbalimbali ikiwemo ya sekta ya Afya,” amesema Kaminyoge.

 

MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI