Na Hamida Ramadhan Matukio Daima app Dodoma
SERIKALI imesisitiza umuhimu wa kuwapima afya ya akili watumishi wa umma kabla ya kuwaajiri, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wanauwezo wa kiakili na kisaikolojia wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Akizungumza leo, Alhamisi Desemba 19, 2024, jijini Dodoma wakati wa kufunga kikao kazi cha siku tatu cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Naibu Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, amesema hatua hiyo inalenga kutatua changamoto za utendaji kwa baadhi ya watumishi.
Sangu ameeleza kuwa changamoto za kisaikolojia zimekuwa zikichangia baadhi ya watumishi kuonyesha tabia zisizofaa kazini, ikiwemo ukaidi, ukosefu wa nidhamu, na kutokubali maelekezo kutoka kwa viongozi wao.
“Hivi karibuni nilikutana na mtumishi wa umma mwenye miaka mitatu kazini, lakini tayari ameanza kuonyesha ukaidi na kukataa kupangiwa kazi. Tabia kama hizi si za kawaida, na mara nyingi huashiria changamoto za kisaikolojia ambazo zinapaswa kushughulikiwa mapema,” amesema Sangu.
Alisisitiza kuwa upimaji wa afya ya akili haupo kwa ajili ya kuminya haki za watumishi, bali ni hatua muhimu ya kuboresha mazingira ya kazi na kuboresha ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi.
Naibu Waziri huyo amewataka viongozi wa idara na taasisi za serikali kuzingatia sera na taratibu za kuboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha watumishi wanapata mafunzo ya mara kwa mara yanayolenga kuimarisha uwezo wao kitaaluma na kisaikolojia.
“Kuwepo kwa tabia zisizofaa kazini huathiri morali ya wafanyakazi wengine na hatimaye kushusha viwango vya utoaji huduma kwa wananchi,” ameongeza Sangu.
Changamoto za Usimamizi wa Sheria na Kanuni
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Selemani Mkomi, amesema kikao hicho kimebainisha changamoto za kutafsiri sheria, kanuni, taratibu, na miongozo ya kinidhamu kwa watumishi wa umma.
“Changamoto kubwa ipo kwenye kushughulikia mashauri ya kinidhamu kutokana na kutoelewa kwa sheria, kanuni, na taratibu huku hivyo Washiriki endeleeni kuzisoma ili kubobea katika maeneo yao ya kazi,” amesema Mkomi.
Hata hivyo Kikao hicho kililenga kuimarisha utawala bora, usimamizi wa rasilimali watu, na utoaji wa huduma bora kwa wananchi ambapo viongozi walisisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya kazi kwa wakati ili kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma.
Mwisho
0 Comments