OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa TAMISEMI imekabidhi bendera ya kijani kwa shule 26 zikiwemo 22 za msingi na nne za Sekondari katika halmashauri nne za wilaya za Mvomero, Morogoro, Kilosa za Mkoani Morogoro na Mufindi Mkoani Iringa baada ya kukidhi vigezo vya kuboresha elimu na mazingira kupitia program ya kimataifa ya Eco-School unaosimamiwa na shirika la kuhifadhi mistu ya asili Tanzania (TFCG).
Programu hiyo ya kimataifa ya Eco-schools imeasisiwa na Taasisi ya Elimu ya Mazingira Duniani TEE, 1994 Copenhagen nchini Denmark zikilenga kuhakikisha jamii na shule zinashirikiana katika upatikanaji wa elimu bora na utunzaji endelevu wa mazingira ili kujenga kizazi chenye mtazamo sahihi kwenye utunzaji wa mazingira, elimu ya vitendo inayokuza ubunifu na kujenga umahiri kuanzia shule za awali, msingi, Sekondari hadi vyuo vikuu.
Akimwakilisha Waziri wa TAMISEMI kutoa bendera hiyo ya kijani katika halfa iliyofanyika shule ya msingi Madizini wilayani Mvomero, Naibu Waziri katika Wizara hiyo anayeshughulikia elimu Mhe Zainab Katimba aliwaelekeza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuhakikisha wanasimamia shule zote zipandwe miti ya kivuli na matunda ili kutengeneza mazingira Bora ya kujifunza na kufundishia
Akasema Walimu, wanafunzi, jamii na wataalamu nao Wana wajibu kuhakikisha miti yote inayopandwa katika maeneo yao inalindwa na kutunzwa ili kudumisha uhifadhi wa ardhi na mazingira.
Akawaagiza viongozi katika shule zilizonufaika kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kusambaza maarifa ya programu hiyo kwa shule zingine za msingi na sekondari na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kila baada ya miezi sita.
Nao Baadhi ya shule wanufaika akiwemo Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kwelikwiji wilaya ya Mvomero, Evance Mwelondo ,mwanafunzi Brighton Kapumwi wa shule ya msingi Kidudwe wilayani humo na Yugnes Davanus wa shule ya msingi Madizini walikiri program hiyo kuwanufaisha ikiwemo kuboresha kilimo, kutunza mazingira, kutumia taka kuzalisha bidhaa na miradi.mingine mingi inayolenga kutunza na kuhifadhi mazingira.
Mwalimu Mwelondo Alisema awali kabla ya mradi, shule hiyo ambayo kwa sasa Ina wanafunzi 807 ilikuwa na muonekano mbovu kimazingira thamani ya shule ilishuka kwenye jamii,mahusiano na jamii yaliyumba hata wanafunzi waliikimbia tofauti na sasa ambapo shule imeongezeka thamani, hawategei Ruzuku ya Serikali kwa asilimia mia Moja,kiwango Cha ufaulu kimeongezeka kutokana na MIRADI.
Akasema kwa sasa Wana miradi 13 ikiwemo ya kilimo cha iliki, vanilla, kokoa, ufugaji nyuki ambapo wana mizinga 26 na shule imekuwa ikinufaika baada ya kuuza mazao na kupata fedha ambazo zinatatua changamoto mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji shirika la kuhifadhi misitu ya asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack alisema Programu ya Eco-schools inatekelezwa katika nchi 87 duniani na inazingatia uhalisia wa mazingira na mahitaji ya nchi ambapo kwa hapa nchini inatekelezwa na kusimamiwa na Shirika hilo kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na upatikanaji wa elimu bora kupitia mfumo wa Elimu kwa maendeleo endelevu.
Aidha akasema programu hiyo ambayo imeendelea kuongeza utayari wa utunzaji wa mazingira na utoaji wa elimu, imekuwa ikiwajengea uwezo walimu na wafanyakazi wa halmashauri za wilaya kutoa elimu bora, kuongeza uelewa na kuunga mkono haki za mtoto hususani za mtoto wa kike za kupata elimu bora.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mvomero Bi Judith Nguli aliahidi wanasimamia vyema program hiyo kutokana na manufaa yake kwa jamii na Mazingira.
Mwisho.
0 Comments