Na Fadhili Abdallah,Kigoma
POLISI mkoani Kigoma wametakiwa kuacha tabia ya kutumia nguvu ikiwemo kuwachapa fimbo waendesha pikipiki maarufu bodaboda wanapowakuta na makosa mbalimbali ya usalama barabarani.
Mwenyekiti wa kamati ya usalama barabarani mkoa Kigoma, Abdulkadri Mushi ambaye aliitisha kikao hicho kuzungumzia vurugu zinazoendelea baina ya pande hizo mbili aliwataka polisi kuacha kukamata watuhumiwa wa makosa ya usalama barabarani kwa kutumia taratibu ambazo hazipo kisheria katika ukamataji.
Sambamba na hilo amewataka waendesha pikipiki hao kufuata taratibu za usalama barabarani ikiwemo kuwa kukamilisha taratibu za vyombo vya moto, kuwa na saiti mila kwenye pikipiki, kuvaa kofia ngumu, kukubali kukamatwa bila shuruti na kufikishwa kituoni wanapotuhumiwa kuwa na makosa na kwamba hiyo yote itaondoa vurugu ambazo .
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa waendesha Bodaboda mkoa Kigoma, Samwel Mtema alisema kuwa tangu kuanza kwa operesheni hiyo vurugu imekuwa kubwa na hakuna mahusiano mazuri baina ya polisi na bodaboda na kwa sababu ya polisi kutumia nguvu ikiwemo kuwachapa fimbo bodaboda hivyo kuwepo kwa matukio ya kupigana baina ya pande hizo mbili yanayoendelea katika wilaya zote za mkoa Kigoma.
Baadhi ya madiwani walioongea kwenye kikao hicho akiwemo Diwani wa kata ya Buhanda Manispaa ya Kigoma Ujiji, Gilbert Kilahumba alisema kuwa polisi wamekuwa wakifanya matendo hayo ya ukamataji na wakati mwingine kuwapiga bodaboda nia kubwa ikiwa kukusanya fedha kutoka kwa waendesha boda boda hao hasa wakati huu wa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Akitoa ufafanuzi kuhusu operesheni hiyo Mkuu wa dawati la polisi jamii mkoa Kigoma, Juma Majula alisema kuwa ni operesheni inayofanyika nchi nzima kwa maelekezo ya Mkuu wa jeshi la polisi nchini na kwamba changamoto za vurugu zinazotokea zinatokana na baadhi ya bodaboda kupinga kukamatwa au kupinga kuchukuliwa pikipiki zao zinapokutwa na makosa.
Hata hivyo Majula alisema kuwa kama kuna changamoto zinazojitokeza katika operesheni hiyo inatokana na hali ya kibindamu ya baadhi ya watendaji hao wa polisi na hivyo baada ya kikao hicho watafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa ili zoezi hilo linalopaswa kukamilika Desemba 31 mwaka huu liweze kuendelea kwa kufuata sheria na taratibu za nchi zilizowekwa.
Mwisho.
0 Comments