Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma Filemon Makungu (kushoto) akizungumza na madereva na makondakta wa mabasi ya abiria katika kituo kikuu cha mabasi mjini Kigoma alipokuwa akifanya ukaguzi kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
POLISI mkoani Kigoma imeendesha zoezi la maalum la kutoa elimu kwa vyombo vya usafiri na usafirishaji kuhusu kuzingatia kufuata sheria za usalama barabarani huku ikikamata baadhi ya vyombo hivyo ambavyo havifuati sheria.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu Desemba 16 alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo nje ya mkoa na nchi Jirani ambapo alizungumza na madereva na watumishi wa magari hao kuhusu kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Akizungumza na wafanyakazi wa mabasi hayo Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma aliwataka wote wanaohusika na kusimamia magari hayo wakiwemo madereva na makondakta kuzingatia sheria za usalama barabara kuhakikisha magari yanafika salama lakini pia kuzingatia sheria nyingine za usafirishaji ikiwemo magari kupaki idadi ya abiria kwa kuzingatia uwezo wa gari na kuacha kukiuka masharti ya leseni zao.
Kamanda Makungu alisema kuwa wakati huu wa kuelekea likizo na sikukuu za mwisho wa mwaka kumekuwa na ongezeko kubwa la abiria jambo linalosabisha magari ya abiria kukiuka sheria na taratibu za leseni zao hivyo kusababisha ajali au usumbufu kwa abiria.
Sambamba na hilo Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma aliingia kwenye magari ya abiria yaliyokuwepo kituoni hapo na kutoa tahadhari kwa abiria kuchukua hatua wanapoona sheria na taratibu za usafirishaji zinavunjwa ambapo alitoa namba yake ya siku na kuwataka abiria kuwasiliana naye wanapoona kuna makosa yanatendeka.
0 Comments