Siku moja baada ya kuvunja Serikali bila kutoa sababu yoyote, Jeshi tawala la Burkina Faso limemteua Waziri Mkuu mpya.
Rimtalba Jean Emmanuel Ouedraogo, Waziri wa Mawasiliano na Msemaji wa serikali iliyopita, ametajwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo.
Kiongozi wa kijeshi, Ibrahim Traore, alitoa tangazo hilo katika amri ya rais iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa.
Mwandishi wa habari wa biashara na mshirika wa karibu wa Traore, Ouedraogo alikuwa Mhariri Mkuu na Mkurugenzi wa televisheni ya taifa ya nchi hiyo.
Hakuna sababu iliyotolewa ya kufutwa kazi kwa Waziri Mkuu wa zamani Apollinaire Joachim Kyelem de Tambela, ambaye aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa muda mara baada ya Traore kunyakua mamlaka mnamo Septemba 2022.
Wanajeshi hao waliuondoa utawala wa kijeshi wa Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba takriban miezi minane baada ya kufanya mapinduzi ya kumuondoa Rais aliyechaguliwa kidemokrasia Roch Marc Kaboré.
0 Comments