MWENYEKITI WA CHADEMA FREEMA MBOWE
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, ametoa maoni yake kuhusu tathmini ya chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa huku akizungumzia changamoto za kisiasa na baadhi ya maneno yanayozungumzwa kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza mbele ya wanahabari leo, Mbowe amepinga baadhi ya tuhuma na maneno yanayohusiana na mgogoro ndani ya chama hicho na kueleza mwelekeo wa CHADEMA kuelekea uchaguzi na maendeleo ya kisiasa nchini.
"Wengine wanalinganisha, nakusema hata Nyerere aling'atuka, Nyerere alikuwa mtumishi wa umma, Rais wa nchi analipwa mshahara, analipwa marupurupu, hafungwi, hashtakiwi, hanyang'ang'anywi mali, anatukuzwa, anaishi kwenye nyumba za umma, sisi wa CHADEMA unaotuona hapa wote hawa wanajitolea," alisema Mbowe.
Mbowe pia, amesema kuwa kuna watu wanatumia mtandao ya kijamii, kueneza maneno yasiyo na msingi, na kushangaa ni kwanini watu hao wanajihusisha na siasa za udanganyifu kupitia mitandao.
"Unasema Mbowe ondoka, watakaoniambia Mbowe ondoka ni wana-CHADEMA, hawa watakaoniambia Mbowe gombea ni wanachama hawa, na viongozi wangu hawa tunaelewana mambo yetu ya ndani yanawahusu nini? Mimi nashangaa tu huko mitandaoni pilipili usiyoila inakuwashia nini?" alihoji Mbowe.
Akijibu suala la mgogoro wa kisiasa na madai ya CHADEMA kutokuwa na mshikamano, Mbowe alisisitiza kuwa Katiba ya chama hicho hairuhusu mtu yeyote kunyimwa nafasi ya kugombea endapo atatimiza masharti ya ndani ya chama.
"Katiba yetu ya chama (CHADEMA) haimzuii mtu yeyote kugombea nafasi, watakaoamua ugombee au usigombee ni viongozi wenzako na wanachama wenzako kwa maelewano," alisema Mbowe.
Mbowe aliongeza kuwa si kweli kwamba kuna ugombanishaji ndani ya chama hicho, akitolea mfano wa mazungumzo yake na Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara.
"Kuna watu wanatamani usiku na mchana waone CHADEMA tunagombana, tunang’oana meno, tunapigana vichwa, hivi nimekaa na Lisu (Tundu Lissu), wanashangaa wamekaa wawili kweli?" alisema Mbowe kwa mshangao.
Kauli za Mbowe zimekuja ikiwa ni siku chache baada ya kuwepo kwa mjadala mkubwa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa CHADEMA na ushiriki wao kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
0 Comments