Na Costantine Mathias, Simiyu.
SERIKALI wilayani Bariadi Mkoani Simiyu imevitaka vikundi vya Wanawake, Vijana na Walemavu kuhakikisha wanarejesha kwa kufuata utaratibu mikopo ya asilimia 10 ambayo wanapewa na serikali ili iweze kunufaisha na wengine.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simoni Simalenga wakati akikabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi mil. 88 katika vikundi 12 vinavyojishughulisha na Kilimo, ufugaji, Upishi na ushonaji.
"Niwapongeze Halmashauri kutimiza takwa la kisheria la kutenga fedha za vijana, Wanawake na walemavu, Mmeweka nguvu kwenye ubunifu wa kuongeza mapato na kufanya fedha za kukopesha vikundi zipatikane...Nia na dhamira ya Rais Samia ni kuwakomboa vijana na Wanawake na walemavu, wakitokea wakajiundia vikundi watakwamisha mikopo" amesema Simalenga na kuongeza.
"Fedha hizi siyo za kwenda kugawana zikazunguke, zirudi ili kila kata ziweze kurejeshwa, robo ya kwanza tumefikia vikundi 12 naamini ndani ya robo 4 tutafikia kata zote...Fedha hizi ni kaa la moto, siyo za kugawana ni za kujikwamua kimaendeleo, tuzitumie fedha hizi vizuri ili zitunufaishe".
Awali, Afisa Maendeleo ya jamii, wilaya ya Bariadi, Beatrice Gwamagobe alisema kuwa jumla ya vikundi 12 vimepewa Mikopo yenye thamani ya shilingi Mil 88 katika robo ya kwanza 2025/26.
Alisema wanatoa Cherehani, vifaa vya Umwagiliaji, Majenereta, Mifugo na vifaa vya Upishi na kwamba katika mikopo hiyo wanawake wamepata yenye thamani ya shilingi mil. 48.5, vijana mil.29 na walemavu mil.10.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Khalid Mbwana alisema kuwa dirisha la maombi limefunguliwa na kuwataka vijana, Wanawake na walemavu kuchangamkie fursa hiyo badala ya kukaa vijiweni kulalamika.
"Tutazingatia maelekezo ya utoaji wa mikopo kwa mujibu wa sheria, hatuna changamoto kwenye marejesho na tutazifikia kata zote zenye vikundi" alisema Mbwana.
Magese Masunga kutoka kikundi cha Mkombozi, Kijiji Cha Nkindwabiye amesema kikundi hicho kinajishugulisha na Kilimo cha Umwagiliaji kwa njia ya matone (drip irrigation) na kuwataka vijana wanaopewa mikopo kitumia vizuri na kuirejesha kwa wakati na wengine wapate.
Minza Lutonja kutoka kijiji cha Mwantimba, Kata ya Matongo amesema kikundi chao wanajishugulisha na Upishi na kikodisha Viti na kwamba wamepewa mkopo wa shilingi Mil.4 ili kujikwamua kiuchumi n kuongeza mtaji katika Biashara yao.
Nyalobi Mabogisi, Mnufaika wa mikopo kutoka kijiji cha Gamboshi amesema kuwa kikundi chao wanajishugulisha na Kilimo cha Umwagiliaji katika mto Duma na Bariadi, hivyo wamepata mikopo ya mitambo ya kumwagilia ili waweze kuendeleza Kilimo chao kwa ufanisi zaidi.
Mwisho.













0 Comments