Header Ads Widget

MAKALA:MWANAHABARI SHALOM ROBERT KIJANA MDOGO ALIYEPATA HESHIMA YA KICHIFU


Na Matukio Daima media 

Katika tukio la kipekee na la kihistoria, Mwanahabari Shalom Robert amepewa heshima ya juu ya kijadi kwa kusimikwa kuwa chifu katika kijiji chake cha Kilosa, kata ya Ihanu, wilaya ya Mufindi mkoani Iringa .

Ikumbukwe kuwa Shalom ni kijana mwenye umri mdogo, amekuwa gumzo baada ya Umoja wa Wazee wa Mila za asili wa kijiji hicho kumuona kuwa kiongozi anayestahili kuwaongoza kwa jina la heshima Chifu KEKOVANGU, jina linalomaanisha “Mkombozi wetu.”


Sherehe hiyo, iliyofanyika mbele ya mamia ya wakazi wa kijiji cha Kilosa, ilitawaliwa na furaha, nyimbo za kitamaduni, na hotuba zilizogusa nyoyo za wengi. 

Wazee wa mila, wakiongozwa na Mzee Ericko Mihale, walimkabidhi Shalom heshima hiyo kwa kauli moja, wakieleza kuwa wanatambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii, hasa kwa vijana Mzee Mihale alisema:

"Kijana sisi wazee kwa umoja wetu tunakusimika leo pamoja na kukupa jina la Chifu KEKOVANGU lenye maana ya Mkombozi wetu. Tunakuombea mafanikio makubwa zaidi hapo baadaye."

Kabla ya kusimikwa uchifu, Shalom alikuwa amefanya ziara fupi kijijini hapo kwa lengo la kujionea maisha ya watu wake na kuchangia maendeleo. Katika ziara hiyo, aliandaa shughuli mbalimbali za kuhamasisha vijana, ikiwa ni pamoja na michezo ya jadi na midahalo ya maendeleo. 

Shughuli hizi ziligusa moyo wa wengi, hasa wazee, ambao waliona bidii na uzalendo wa Shalom kama kijana wa kizazi kipya mwenye maono ya kuleta maendeleo.

Akizungumza baada ya kupokea heshima hiyo, Shalom alisema kuwa heshima hiyo ni kubwa kwake na hajawahi kuwa na ndoto za kuja kupata.

"Sikutarajia heshima hii kubwa kutoka kwa wazee wa mila. Nimeguswa na heshima hii, na naahidi kuendelea kuwatumikia watu wangu kwa hali na mali. Uchifu huu ni mwito wa kuwatumikia zaidi."



Hata hivyo waswahili husema penye nia Pana njia hivyo kwa  muda mrefu, Shalom Robert amekuwa akihamasisha maendeleo ya kijamii kupitia taaluma yake ya uandishi wa habari na uhamasishaji wa vijana.

 Kupitia vipindi vyake vya redio na televisheni mbali mbali ameendelea kuwa chachu ya mabadiliko, akihimiza vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Katika kijiji cha Kilosa, alihamasisha uanzishwaji wa timu za michezo ili kuwapa vijana ajira na kuwafanya waepukane na vitendo vya uhalifu. 

Wazee walikiri kuwa juhudi hizi zimetoa matokeo chanya, na sasa kijiji kimeanza kuona mabadiliko makubwa katika mtazamo na mienendo ya vijana.

"Kwa muda mfupi aliofanya kazi na sisi, tumeshuhudia mabadiliko. Vijana wetu wameanza kuthamini utamaduni wetu na wanajihusisha zaidi na shughuli za maendeleo," alisema Mzee Jesca Ndunguru, mmoja wa wazee wa mila wa kijiji hicho.

Kusimikwa kwa Shalom Robert kuwa Chifu KEKOVANGU si tu heshima kwake binafsi, bali ni ujumbe kwa vijana wote kuwa jamii inatambua mchango wao.

Hivyo  tukio hili limewafundisha vijana kuwa juhudi, bidii, na uzalendo vinaweza kuleta heshima na nafasi ya uongozi, hata kwa kizazi kipya.

Shalom alisema kuwa anapanga kuanzisha mradi wa maendeleo ya kijamii katika kijiji cha Kilosa kama sehemu ya kuwashukuru wazee kwa imani waliyoonyesha kwake.

 Mradi huo utalenga kuboresha miundombinu ya kijiji, elimu, na michezo.

"Nitatumia nafasi hii kushirikiana na watu wangu kuleta maendeleo. Nafasi hii ni fursa ya kujifunza na kuonyesha mshikamano na jamii yangu," alisisitiza Shalom.

Tukio hili lilihitimishwa kwa sherehe za kitamaduni zilizowahusisha wakazi wa Kilosa na wageni waliokuja kushuhudia tukio hilo la kihistoria. 

Nyimbo na ngoma za jadi zilihanikiza hewani, na watu walijipatia chakula cha pamoja kama ishara ya mshikamano.

Wazee wa mila walieleza kuwa kusimikwa kwa Shalom ni sehemu ya juhudi zao za kurithisha vijana utamaduni wa heshima, maadili, na uongozi wa kizalendo.

 Walitoa wito kwa viongozi wengine wa vijana kuiga mfano wa Shalom wa kuwa mstari wa mbele katika masuala ya maendeleo.

Kusimikwa kwa mwanahabari kijana kama Chifu ni tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa mara nyingi katika jamii ya Kilosa. 

Hakuna unaishi kuwa hii inaonyesha jinsi jamii ya sasa inavyoweza kuvuka mipaka ya umri na jinsia katika kutambua viongozi bora.

Shalom Robert sasa anakumbatiwa kama mfano wa kijana anayeweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii yake.

 Wazee wa mila walimwambia kuwa wanatarajia kuona zaidi kutoka kwake, si tu kwa kijiji cha Kilosa, bali pia kwa jamii pana ya Tanzania.

Kupitia tukio hili limeacha funzo kubwa kwa jamii. Kila mmoja ana nafasi ya kuchangia maendeleo, bila kujali umri, jinsia, au taaluma.


Kutokana na heshima aliyopata Shalom Robert ni mwaliko kwa vijana wengine kushiriki katika kuboresha maisha ya watu wao.

Shalom, sasa Chifu KEKOVANGU, ameonyesha kuwa uongozi ni zaidi ya vyeo rasmi – ni kuhusu kujitoa, kujali, na kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto za jamii. Kwa heshima hii mpya, bila shaka Shalom atazidi kuwa sauti ya matumaini kwa Kilosa na kwingineko.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI