Na Hamida Ramadhan Matukio Daima app DODOMA
WATANZANIA wametakiwa kuchukua hatua madhubuti katika matumizi ya nishati safi kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda mazingira na kuendeleza uchumi wa nchi.
Wito huu ulitolewa na Dkt. Kenneth Nzowa, Mkuza Mtaalamu Mwandamizi kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania,wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Kongamano la 16 la Wanazuoni lililofanyika katika Chuo cha Serikali za Mitaa, Kampasi Kuu ya Hombolo jijini Dodoma.
Katika kongamano hilo mada kuu ilikuwa "Nishati Safi, Changamoto Zilizopo na Uwezekano wa Kuhamasisha Wananchi Kufanya Kama Sehemu ya Maendeleo Yao."
Dkt. Nzowa amesema kuwa matumizi ya nishati safi ni hatua muhimu katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya nchi, kwani nishati safi kama vile umeme wa jua (solar) na gesi ni rafiki kwa mazingira na inachangia katika kuboresha maisha ya Watanzania.
Ameeleza kuwa, licha ya changamoto za gharama za vifaa kama vile paneli za sola, wananchi wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na vikundi vya kijamii kama vile SACCOS ili kupata mikopo ya kununua vifaa vya nishati safi.
Ameongeza kuwa, Serikali inapaswa kuangalia namna ya kupunguza kodi kwenye viwanda vya sola ili kufanya nishati safi iweze kupatikana kwa urahisi zaidi kwa wananchi.
Aidha, Dkt. Nzowa amesisitiza umuhimu wa elimu kwa umma kuhusu faida za nishati safi.
Ameweka wazi kwamba, vijijini, bado kuna uelewa mdogo kuhusu matumizi ya nishati safi, hivyo ni muhimu kutoa elimu kwa watu ili waelewe jinsi nishati hii inavyoweza kuboresha maisha yao, kwa mfano, katika matumizi ya majiko ya gesi kwa kupikia na umwagiliaji wa mashamba kwa kutumia umeme.
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri, Prof. Magreth Bushesha, amesema kuwa kongamano hili ni muhimu kwa sababu linawaleta pamoja wanazuoni kutoka vyuo mbalimbali, wakiwa na jukumu la kutoa mchango wao katika kutatua changamoto zinazokumba jamii, hasa katika suala la matumizi ya nishati safi.
Amesisitiza kuwa, nishati safi inahamasishwa ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanaendana na mabadiliko ya ulimwengu wa kisasa, huku ikizingatia pia ulinzi wa mazingira.
Naye, Mwanafunzi wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu, Nicholaus Rugarabamu, ambaye alipata tuzo ya Mwanafunzi Bora, alisema anajivunia mafanikio yake, ambayo ameyapata kutokana na juhudi zake za kusoma kwa bidii na kushirikiana na wenzake.
Amesisitiza kuwa siri ya mafanikio ni kujituma, kusikiliza walimu, na kumtanguliza Mungu katika kila jambo.
Hivyo, kongamano hili limeonyesha umuhimu wa kushirikiana kama jamii katika kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanaenezwa kwa ufanisi, huku kila mmoja akichukua jukumu la kuboresha mazingira yake na kuchangia katika maendeleo ya taifa.
Mwisho
0 Comments