IBADA YA KRISMASI KITAIFA IRINGA HIZI HAPA SALAAM ZA CCT MKOA WA IRINGA
Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi
wake.
Zaburi 33:12
Kwa niaba ya CCT MKoa na kwa niaba ya Jumuiya nzima ya CCT,
Nichukue nafasi hii, kumshukuru Mungu kukutana leo kama hivi tulivyo
kwa umoja wetu. Tulipanga na Mungu ameruhusu litokee. Penye umoja
pana nguvu.
Tunamshukuru Mungu kwa neema, amani na utulivu uliopo katika Nchi
yetu nzuri Tanzania,
Nimpongeze Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri jeshi mkuu, kwa uongozi wake mzuri
yeye na wasaidizi wake wote katika Serikali. Tumpongeze kwa kazi
kubwa zinazoonekana na zisizoonekana. Baadhi ya kazi zinazoonekana ni
kama Uwekezaji mkubwa wa miradi ya kimkakati na uendelezaji wa
miradi iliyokuwepo tumeona miradi mingi ikiendelea kukamilishwa,
baadhi yake ni;
a. Ukamilishaji na uendelezaji wa Reli ya mwendokasi (SGR) kutoka
Dar hadi Dodoma. Kwa treni hii unatumia muda mfupi sana kwa SGR
ni muda mfupi tu, niwasihi wakristo wenzangu na watanzania wote
kwa ujumla, tuilinde miradi hii na kuitunza.
b. Ukamilishaji na uendelezaji wa Bwawa la umeme la Mwalimu Julias
Nyerere.
c. Uwekezaji unaoendelea katika sekta ya elimu na afya ni mkubwa.
Kikubwa na chenye mguso, hivi karibuni tumeshuhudia uzinduzi wa
vifurushi vipya vya Bima ya afya kwa makundi kadhaa. Ni hatua
nzuri. Nchi yoyote inayojali watu wake, inawekeza kwenye afya,
maendeleo na usalama wao katika Nyanja zote.
1Pongezi:
a. Nimpongeze Rais na vyombo vyote vinavyohusika kwa Uchaguzi wa
Serikali za mitaa. Pia, asanteni Watanzania wote walioshiriki
kikamilifu katika zoezi hilo. Katika maisha jambo la kuchagua ni
jambo la wajibu. Hatuwezi kukwepa kuchagua na hatuwezi kukwepa
uchaguzi.
b. Nimpongeze Dkt. Tulia Ackson spika wa Bunge, kuwa Spika wa
kwanza kutokea ukanda wetu huu pendwa wa Afrika kuchaguliwa
kuwa Rais wa umoja wa maspika Duniani, Dkt. Tulia ni kiongozi
mzuri mwenye kujiamini na MUNGU amempa neema ya kuwa na
vipawa vingi katika maisha yake, sisi tunazidi kumwombea katika
nafasi zake zote za kiuongozi alizonazo pamoja na wabunge wote
wa Tanzania watekeleze wajibu wao kwa kumtanguliza Mungu, na
wabunge wote waliofanya kazi yao ipasavyo majimboni mwao,
Mungu awape kibali cha kurejea Bungeni tena katika uchaguzi ujao.
c. Nipongeze vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na mihimili yote kwa
ushirikiano walionao kati yao nasi. Ijapokuwa ni wajibu wao, ila sisi
kama Watanzania tuna kitu cha pekee cha kuishi kama ndugu na
jamaa wamoja tukisaidiana na kuwasiliana katika mambo mengi
yanayotusibu. Asanteni kwa kutuhakikishia kuwa tupo salama wakati
wote na hata kipindi hiki cha sikukuu. Sisi kama kanisa
tunawaombea katika kazi yao Mungu awe upande wao, hofu ya
Mungu iwe mioyoni mwao katika kila maamuzi wafanyao kwa
kufuata sheria za Nchi.
Baadhi ya Changamoto
a. Uchaguzi wa serikali za mitaa umeisha. Niwapongeze watanzania
wenzangu kwa uchaguzi uliopita wa Serikali za mitaa, ninaimani kila
mtu ametumia haki yake ipasavyo kugombea na kuchagua kiongozi
amtakaye, hongera kwa waliochaguliwa wakaifanye kazi yao
ipasavyo na Mungu awasaidie. changamoto kadhaa zilizojitokeza
zifanyiwe kazi na wahusika wa pande zote ili wakati mwingine
zisijirudie, na ili tuwe na taifa ambalo haki itakuwa ndiyo msingi
mkuu.
2Bado nchi yetu ni kwa sehemu kubwa ya Watanzania ni Wakulima
wadogo na wafanyabiashara wadogo. Miaka miwili mitatu tumekuwa
na ruzuku ambayo imesaidia wengi wa wakulima na
wafanyabiashara hasa wa hali ya chini. Niombe serikali yetu sikivu
iendelee kuweka mazingira mazuri ya wakulima wadogo na
wafanyabiashara wadogo ili wafanye kazi katika maeneo yaliyo
salama, yaliyopangwa na yenye kuwaletea uhakika wa kesho ya
maisha yao.
c. Vipato vya watanzania wengi si vikubwa. Na changamoto kubwa
tunayoona ni Watanzania kukosa uwezo wa kumudu gharama ya
matibabu katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na ngazi ya familia.
Naomba kukumbusha kuwa ile ahadi ya Bima ya afya kwa watu wote
ingeweza kuwa mkombozi mkubwa kwa watu wengi. Hata hivyo,
kumeendelea kuwa na wadau kadhaa wanaosadia kupata fedha kwa
namna mbalimbali kuwezesha matibabu ya baadhi ya wenye
changamoto. Watanzania wanapendana, bado nchi yetu ni nchi
nzuri.
d. Hali ye hewa ya mwaka huu, ina kila dalili za kuwa mvua si nyingi ya
kutosha kuvumilia mazao ya muda mrefu kama tulivyozoea. Wito
wangu kwa serikali, itusaidie kupata mbegu za aina nyingi
zinazoweza kustahimili mvua za muda mfupi, ili mwaka unaofuata
tuwe na chakula kwa kuwa eneo letu bado ni eneo la uzalishaji wa
mazoa ya chakula.
Wito wangu.
a. Pia niwakumbushe Watanzania, kwa kuwa ibada ya Christmas
itakayofuata itakuwa ni baada ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025
naomba tuombee uchaguzi ujao, ili MUNGU atuletee viongozi wenye
sifa na wanaohitajika kwa majira na nyakati tulizonazo, sisi kama
kanisa wajibu wetu mkubwa ni kuomba na kushauli, na hilo
hatutaacha kufanya hivyo kila wakati!
b. Katika kipindi hiki, tufanye kazi kwa nguvu, kwa roho na kwa akili
zote kwa kuwa kazi ni ibada. Tupunguze muda wa sherehe,
tuongeze muda wa kufanya kazi.
c. Tumwabudu Mungu wetu katika Roho na kweli, ili Mungu apate
kutukuzwa katika Kanisa, jamii yetu na familia zetu. Mungu ni Roho,
imetupasa kumwabudu katika Roho na Kweli. Mungu anapotukuzwakatika Roho na kweli ndipo maendeleo ya kweli yanapotokea kwa Kanisa na nchi nzima. Mungu anapenda kuabudiwa katika hali ya uzuri wake, utakatifu na mpangilio mzuri. Tuwe na ibada zenye uchaji zinazoandaliwa vizuri kutoka ngazi ya familia.
d. Kipindi hiki kuna roho za udanganyifu nyingi. Huduma za udanganyifu na kazi za udanganyifu ni nyingi sana. Tukae kwa tahadhari na tuishi kwa tahadhari.
e. Tusiache kuheshimiana, kunyenyekeana na kufanya kazi kwa Bidii. Hata kama Yesu anakuja kesho asubuhi, atukute tukiendelea na Ibada, atukute tukifanya kazi. Usifunge duka kwa sababu umeambiwa Yesu anakuja.
Nitoe tahadhari pia, katika nyakati hizi za mwisho, tutasikia mambo mengi sana yanayohusiana na ujio wa Yesu mara ya pili. Tusome Neno, tufike katika nyumba za Ibada, tuongeze toba na ibada. Nyakati hizi pia, vitendo viovu vimeendelea kuongezeka kwa wazi. Kumekuwa na ongezeko la matendo ya imani za kishirikiana na viashiria vya ushirikina katika jamii zetu, vitendo kama uvunjaji wa nazi kwenye jamii, vitendo vya ubakaji kwa watoto wadogo, vitendo vya aibu na udhalilishaji wa kijinsia kwa namna mbalimbali. Ni dalili za watu wasio na Yesu na jamii zisizo starabika katika ulimwengu uliobadilika sana. Tukemee tabia hizi kwa njia zote za sala na mifumo yetu ili Yesu akute jamii iliyoandaliwa na kanisa lililotayarishwa kwa ajili ya ujio wake.
Tunapoingia mwaka 2025, mwambie Mungu vitu ambavyo hukuweza kufanikiwa, sekta ambazo hukufaulu kwa mwaka 2024, mwambie Mungu naomba nifanikishe kwa viwango ambavyo wewe Mungu unataka nifanikiwe.
Aidha, nichukue fursa hii kumshukuru Mungu kwa amani tuliyonayo katika nchi yetu ya Tanzania, na kuliombea Taifa letu, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia S. Hassan na wote wanaomsaidia.
Nawatakia Baraka tele katika Krismas ya mwaka 2024 na katika kuumaliza mwaka 2024. Mbarikiwe sana. Amen.
Askofu Dkt. B. Gaville
Makam mwenyekiti wa CCT Mkoa wa Iringa na Askofu
KKKT- Dayosisi ya Iringa
0 Comments