Mkutano Mkuu wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN) umefungua ukurasa mpya wa uongozi baada ya wajumbe wa mkutano huo kumchagua Edwin Soko kuwa Mwenyekiti mpya wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Soko anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Salome Kitomari, ambaye ameiongoza MISA-TAN kwa mafanikio makubwa kwa kipindi cha miaka nane tangu mwaka 2018.
Uchaguzi huu uliofanyika katika ukumbi wa UCSAF, jijini Dodoma, umeonesha mwelekeo mpya wa taasisi hiyo katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na haki za wanahabari nchini Tanzania na katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Katika uchaguzi huo, Edwin Soko alitangazwa mshindi na Ali Aboth, Msimamizi wa Kamati ya Uchaguzi, baada ya kupata kura 33, akiwapiku wapinzani wake Said Mmanga, aliyepata kura 9, na Betty Masanja, aliyepata kura 3. Kati ya kura 46 zilizopigwa, kura moja iliharibika.
Mwenyekiti mpya, Edwin Soko, ameahidi kuendeleza agenda za MISA-TAN kwa kuhakikisha masuala ya uhuru wa habari na usalama wa wanahabari yanapewa kipaumbele, huku akitoa shukrani kwa wajumbe wa mkutano kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuongoza taasisi hiyo.
Taasisi ya MISA-TAN imekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kukuza haki za vyombo vya habari na wanahabari, na kuchaguliwa kwa Edwin Soko kunatarajiwa kuimarisha juhudi hizi zaidi kwa manufaa ya tasnia ya habari nchini na ukanda mzima wa Kusini mwa Afrika.
0 Comments