MKAZI wa Mtaa wa Mbwate Kata ya Mkuza Wilayani Kibaha Godfrey Killu (30) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauji ya aliyekuwa mke wake Elizabeth Sindakila (26) kwa kumpiga na fimbo akimlazimisha kurudi nyumbani wakitokea kwenye kilabu cha pombe.
Kamanda wa Polisi Mkoawa Pwani ACP Salim Morcase amesema kuwa marehemu alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi.
Morcase amesema kuwa Polisi ilipata taarifa Desemba Mosi mwaka huu majira ya saa 5:00 asubuhi huko hospitali ya Tumbi baada ya muhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kutoa taarifa kuhusu marehemu.
Amesema kuwa walipata taarifa kutoka kwa mhudumu huyo kuwa marehemu alifariki alipokuwa akipatiwa matibabu ya majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na baada ya kupokea taarifa hizo jeshi la Polisi lilifika hospitalini hapo na kupata maelezo ya kina.
Aidha amesema kuwa baada ya kupata taarifa hizo lilifanya utaratibu wa kumkamata mume wa marahemu kwa mahojiano ambapo alikiri kuhusika na kifo cha mkewe huyo kwa kumpiga na fimbo akimlazimisha kurudi nyumbani wakitokea kwenye kilabu hicho cha pombe.
mwisho
0 Comments