Wasimamizi wa vituo vya uchaguzi wametakiwa kuwa makini na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, na Taratibu za uchaguzi ili kuepuka vitendo vya rushwa, ambayo ni kikwazo kikubwa katika mchakato wa kupata viongozi waadilifu na bora.
Wito huu umetolewa na Sospeter Tyeah, Afisa wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, ambaye ametoa semina muhimu kwa wasimamizi wa uchaguzi wilaya ya Mbeya Vijijini. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Malanatha na yalihudhuriwa na zaidi ya wasimamizi 2,000 kutoka kata mbalimbali za wilaya hiyo.
Katika semina hiyo, Tyeah alisisitiza umuhimu wa uadilifu na usafi wa kiutendaji katika kipindi chote cha uchaguzi, akisema kwamba rushwa ni tatizo linalo athiri utawala bora na ustawi wa jamii.
"Wasimamizi wa uchaguzi mna jukumu kubwa la kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki, wazi na salama. Kama mkitumika kwa njia ya rushwa, mtachangia kuharibu demokrasia na kuleta viongozi wasio na maadili," alisema Tyeah.
Aliongeza kuwa, wasimamizi wanapaswa kuwa mifano bora ya uaminifu na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Afisa huyo wa Takukuru alifafanua kuwa rushwa siyo tu kwamba inashusha hadhi ya uchaguzi, bali pia inachochea migogoro, kutokuelewana na kupunguza imani ya wananchi kwa mfumo wa uchaguzi.
Aidha, aliwataka wasimamizi hao kutambua kuwa wao ni sehemu muhimu ya kuhakikisha kwamba kila kura inahesabiwa kwa ufanisi na kwa haki inamchango mkubwa kwenye jamii, na kwamba kila mchakato wa uchaguzi unatekelezwa kulingana na sheria na miongozo iliyowekwa.
Tyeah pia aliwahimiza washiriki wa semina hiyo kutumia elimu waliyopata kutokomeza rushwa kwenye majukumu yao ya usimamizi, na kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya rushwa katika jamii zao. Alikumbusha kuwa Takukuru iko tayari kushirikiana nao ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa njia ya haki, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekutwa akijihusisha na vitendo vya rushwa.
"Elimu mnayopata leo ni muhimu sana. Kila mmoja wenu anawajibika kuhakikisha kwamba taratibu na sheria zinazingatiwa katika kila hatua ya uchaguzi, hakuna nafasi kwa rushwa kuingia. Tunataka viongozi wakiingia madarakani kwa njia ya haki na kwa mapenzi ya wananchi, si kwa njia ya udanganyifu na hongo," alisisitiza.
Semina hiyo ililenga kuongeza ufanisi katika maandalizi ya uchaguzi na kupambana na rushwa kwa kuhakikisha kwamba wasimamizi wa uchaguzi wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya taratibu, sheria, na kanuni zinazohusu uchaguzi. Kwa kufanya hivyo, Tyeah alisema, wataweza kutoa mchango muhimu katika kuhakikisha uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia unafanyika, na kwamba kila mtanzania atapata fursa ya kuchagua kiongozi mwenye sifa na uwezo wa kuwatumikia.
Katika hatua nyingine, washiriki walieleza kuridhishwa na elimu waliyoipata, na walisisitiza kwamba watatumia maarifa hayo kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao, kwa kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki, na bila vitendo vya rushwa.
0 Comments