Header Ads Widget

UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA: TWENDENI TUKACHAGUE VIONGOZI BORA KUTOKA CCM – MNEC SALIM ASAS

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Salim Abri Asas, ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27. 

Akizungumza na wanawake wafanyabiashara ndogondogo, Asas alisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi bora kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Katika hotuba yake, Asas aliwakumbusha wanawake kuhusu mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu. Alieleza kuwa serikali ya CCM imekuwa mstari wa mbele katika kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo hiyo, ambayo ni sehemu ya juhudi za chama katika kupunguza umaskini na kuinua hali ya maisha ya wananchi.

“Hili ni jukumu letu sote kuhakikisha mikopo hii inaendelea kuwanufaisha watu wengi zaidi. 

Kuwa hii  inawezekana tu ikiwa tutawachagua viongozi waadilifu, wenye uwezo wa kusimamia rasilimali zetu na kutekeleza ilani ya CCM kwa ufanisi,” alisema Asas.

Aliongeza kuwa ili maendeleo ya kweli yaweze kufikiwa, ni lazima wananchi wawe na viongozi wanaowajibika na wanaoweza kuwaunganisha na fursa mbalimbali, ikiwemo mikopo na miradi ya maendeleo. Alisisitiza kuwa chama chenye ilani madhubuti kama CCM ndicho chenye uwezo wa kuleta maendeleo endelevu.

MNEC Salim Asas aliwahimiza wananchi waende kwa wingi kupiga kura na kuchagua viongozi kutoka CCM ambao wataendeleza juhudi za kuleta maendeleo, kusimamia uwajibikaji, na kuhakikisha fursa zinawafikia wananchi wote.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI