Na Asha Athuman, Mbeya
WAKATI watanzania wanajiandaa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 viongozi wa dini na wananchi mkoani Mbeya waingiwa na hofu ya vitendo vya Rushwa kutawala .
Ikumbukwe kuwa uchaguzi huu unaoratibiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ni hatua muhimu kwa demokrasia ya nchi na maendeleo ya jamii.
Uchaguzi ambao utahusisha kuchagua viongozi wa ngazi mbalimbali, kama vile wenyeviti wa vijiji ,wenyeviti wa serikali za mitaa na vitongoji, na wajumbe wa halmashauri za vijiji
Uchaguzi huu ni sehemu ya kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowaamini kuwa na uwezo wa kusimamia maendeleo ya kijamii na kisiasa. Raia wenye umri wa miaka 18 wanaruhusiwa kupiga kura, huku wale wa miaka 21 wakiwa na sifa za kugombea uongozi.
Viongozi watakaochaguliwa wanatarajiwa kuwa msingi wa utekelezaji wa sera na maendeleo kutoka ngazi za kijiji hadi taifa.
Hata hivyo, hofu ya vitendo vya rushwa imeanza kujitokeza, hali ambayo imewatia wasiwasi wananchi na viongozi wa dini ambao wanaona hatari ya demokrasia kuharibiwa na vitendo vya ufisadi.
Rushwa imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika kipindi cha uchaguzi, ambapo wagombea au wapambe wao hutumia mali kama fedha, pombe, nguo, au zawadi nyingine kuwashawishi wapiga kura. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili, rushwa ni tendo la kutoa au kupokea kitu cha thamani ili kupata upendeleo fulani, jambo ambalo linaleta athari mbaya kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi.
Katika muktadha wa kisheria, rushwa ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007. Rushwa pia imekemea kupitia maandiko ya kidini, ambapo vitabu kama Biblia na Qur'an vinaitaja kama dhambi kubwa inayoharibu maadili na kuleta uharibifu wa jamii.
Emmanuel John, mkazi wa Kata ya Ilomba, Mbeya, amewataka wananchi kutokubali kushawishiwa kwa rushwa na badala yake kumchagua kiongozi anayewasilisha hoja zenye tija. “Kiongozi anayekushawishi kwa rushwa hana uwezo wa kuleta maendeleo; anatumia mbinu hizo kuficha udhaifu wake,” alisema.
Mariamu Said, mfanyabiashara wa soko la Sido, Mbeya, alihimiza utoaji wa elimu zaidi kuhusu athari za rushwa kwa wanawake, akisema: “Tunahitaji viongozi wenye utashi wa kusimamia ajenda za wanawake, si wale wanaotumia rushwa.”
Askofu Donald Mwanjoka wa Kanisa la TAG Mbeya alionya kuwa kiongozi anayepatikana kwa rushwa ni mwovu na hana kibali cha Mungu. Alisisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kutumia nafasi zao kukemea vitendo vya rushwa.
Sheikh Hassan Katanga wa Baraza la Masheikh Mbeya aliongeza kuwa kiongozi wa aina hiyo ni adui wa maendeleo na hafai kuaminiwa na wananchi. “Rushwa inaonyesha udhaifu wa uongozi; tunapaswa kuwakataa viongozi wanaotumia njia hiyo,” alisema.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo, alisema taasisi yake imejipanga kukabiliana na vitendo vya rushwa kupitia elimu kwa umma, mikutano ya hadhara, na klabu za wapinga rushwa. Alisisitiza kuwa sheria inakataza wagombea kutoa misaada miezi sita kabla ya uchaguzi, isipokuwa kwa dharura.
Aliwahimiza wananchi kuwa makini na wagombea wanaotoa zawadi kama njia ya kujinufaisha kisiasa.
“Takukuru ipo macho muda wote, na hatua kali zitachukuliwa kwa wale wanaojihusisha na rushwa,” alisema Ndimbo.
Kumbuka wananchi wanapaswa kutambua haki zao za msingi na kuchagua viongozi kwa misingi ya uwezo na uadilifu badala ya kushawishiwa na rushwa.
Tambua Demokrasia ya kweli na maendeleo endelevu vinawezekana tu pale ambapo jamii inakataa rushwa na kuwajibika kwa pamoja katika mchakato wa uchaguzi.
0 Comments