Wafanyabiashara za mazao na nafaka wanaofanya biashara ya kuvuka mpaka
Dk.Chaboba Mkangwa Afisa tathmini na ufuatiliaji TCCIA Kigoma akitoa repoti ya utafiti alioufanya kuhusu vikwazo vikwazo vya kikodi vinavyowakabili wafanyabiashara wa mazao wanaofanya biashara ya kuvuka mpaka
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Chama Cha Wafanyabiashara, wenye viwanda na Kilimo (TCCIA) kimeainisha vikwazo 18 visivyo vya kikodi ambavyo vimekuwa changamoto kubwa na kuzuia kukua kwa biashara ya kuvuka mpaka kwa wafanyabiashara za mazao na nafaka nchini Kwenda katika nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki.
Meneja ufuatiliaji na tathmini (TCCIA) mkoa Kigoma, Dk.Chaboba Mkangwa alisema hayo akitoa taarifa ya utafiti waliofanya kwenye vituo vinne vya ushuru wa forodha nchini vinavyoshughulikia taratibu za kuvuka mpaka.
Dk.Mkangwa akiwasilisha ripoti kwa wadau wanaohusika na biashara na usafirishaji wa mazao nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya mradi wa Kukuza Biashara kwa wafanyabiashara wa ndani kwenda katika nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki kwa Kushughulikia Vikwazo Visivyo vya kikodi (NTBs) kwenye Biashara za mazao na nafaka mradi unaofadhiliwa na Bodi ya mageuzi ya kijani Afrika (AGRA) na Taasisi ya Bill and Mellinda Gates ya Marekani.
Alisema kuwa katika utafiti huo walioufanya katika hivyo vya forodha alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni Pamoja na malalamiko ya tozo na kodi zinazotozwa mara mbili, wanunuzi katika nchi nyingine za Afrika Mashariki kupanga bei badala ya bei kupangwa na mwenye bidhaa , gharama za uendeshaji kuwa juu, tuhuma za rushwa na hongo na changamoto za uelewa mdogo kwa wafanyabiashara wa usafirishaji bidhaa nje na uingizaji biashara nchini
Sambamba na hilo alisema kuwa wafanyabiashara wengi wanakabiliwa na changamoto ya kutojua lugha kwa nchi wanazoenda kufanya biashara, rushwa na urasimu katika kupata vibali, kutokuwepo kwa masoko ya Pamoja kwenye maeneo mengi ya mipakani na masoko yasiyoaminika, serikali kuzuia baadhi ya mazao kuuzwa nje bila kuwepo taarifa rasmi kwa wafanyabiashara.
Akizungumza katika mkutano huo Katibu wa TCCIA mkoa Kigoma, Prosper Guga alisema kuwa mradi huo unalenga kuibua na kuaninisha vikwazo visivyo vya kikodi vinavyowakabili wanawake na vijana wanaofanya biashara ya mazao Kwenda nje ya nchi ili kukabiliana na vikwazo hivyo kuwezesha kuongeza ukubwa wa biashara ya kuvuka mpaka inayofanywa na wanawake na vijana.
0 Comments