Header Ads Widget

TAKUKURU: MAPUNGUFU KWENYE MIRADI TATIZO KUBWA KIGOMA


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa Kigoma imesema kuwa bado utekelezaji wa miradi mbalimbali ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa Kigoma imeendelea kukabiliwa na mapungufu makubwa licha ya kazi kubwa wanayofanya kutoa ushauri kuhusiana na utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuzingatia  viwango.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma, John Mgallah akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari ya utekelezaji ya taasisi hiyo kwa  robo mwaka kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu alisema kuwa jumla ya miradi 35 yenye thamaani ya shilingi Bilioni 18.6 ilifanyiwa mapitio ambapo kati yake miradi 19 yenye thamani ya shilingi Bilioni 7.7 ilikutwa na mapungufu.


Mgallah alisema kuwa miongoni mwa mapungufu hayo ni Pamoja na kutozingatiwa kwa sheria za manunuzi, kutozingatiwa kwa taratibu za ujenzi ikiwemo kutozingatiwa kwa ramani za majengo, kuchelewa kwa miradi na baadhi ya nyaraka muhimu za utekelezaji wa miradi ikiwemo mihutasari ya kutoa fedha, nyaraka za kupokea vifaa kutoonekana.

Naibu Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa Kigoma alitoa mfano wa ujenzi wa kituo cha polisi Halmashauri ya wilaya ya Kasulu uliogharimu shilingi milioni 114 ambapo ujenzi wa jengo hilo hauendani na ramani iliyokuwepo.

Aidha katika mradi mwingine aliutaja mradi wa ukarabati wa hospitali ya Mji wa Kasulu wenye thamani ya shilingi milioni 900 ambaapo ukarabati uliofanyika kwenye baadhi ya majengo hauendani na michoro iliyoandaliwa, uwepo wa mbao zisizo na ubora na overhang ya bati nje ya za majengo kuwekwa kwa milimeta 300 badaala ya milimeta 600.


Kufuatia mapungufu hayo Naibu Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa Kigoma alisema kuwa wametoa ushauri kwa mamlaka zinazosimamia miradi hiyo kuhakikisha mapungufu yanafanyiwa kazi na kwamba tayari katika baadhi ya miradi mapungufu hayo yameanza kurekebishwa.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI