-Sasa mizani mitatu kupelekwa haraka, atoa maelekezo mahususi kwa Katibu Mkuu na Tanroads.
Na Moses Ng'wat, Mbozi.
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashingwa, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi, Aisha Amour, kutafuta haraka fedha zilizoombwa na Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Songwe kwa ajili ya kukamilisha awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa kituo cha kuegesha magari ya mizigo (Malori) katika eneo la Chimbuya, Wilayani Mbozi.
Ameeleza kuwa mradi huo unaotekelezwa na Tanroads Mkoa wa Songwe kwa gharama ya shilingi bilioni 2, tayari serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.8 ambazo zimeendelea kutumika
Waziri Bashungwa ametoa maagizo hayo, leo Novemba 18, 2024 alipotembelea na kukagua mradi huo ambao unatekelezwa kwa awamu ya kwanza wakati wa ziara yake ya siku moja Mkoani Songwe kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo.
Amesema kuwa, mradi wa maegesho wa Chimnuya ni miongoni mwa miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali kwa ajili ya kutatua changamoto kubwa ya msongamano wa Malori yaendayo nje ya nchi katika Mji wa mpakani wa Tunduma na pindi utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuegesha malori 600.
"Meneja wa Tanroads mimi nimeshakuja hapa na kujionea maedeleo ya mradi huu, naomba kasi iongezeke na ili kufikia wiki ya kwanza ya mwezi Disemba mradi huu uanze kutoa huduma, hivyo nimuagize Katibu Mkuu wa Wizara kutafuta fedha haraka ili ujenzi wa awamu ya kwanza ukamilike" alisema Bashungwa.
Pia amemuelekeza Katibu Mkuu huyo kuhakikisha anatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa awamu ya pili ya mradi huo, huku akishauri mkandarasi anayrtekeleza mradi apewe pia mradi wa awamu ya pili.
Kadhalika, Waziri Bashungwa amemuagizaMkurugenzi wa Matengenezo wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Makao Makuu, Mhandisi Dkt. Christina Kayoza, kufika mara moja mkoani Songwe kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kusimamia maelekezo yote aliyoyatoa.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashungwa ameelekeza kuwa hadi kufikia Novemba 20, 2024 watendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha wanapeleka mizani ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo (Mobile weigh Brudge) katika eneo la Mpemba katika Mji mdogo wa Tunduma ili kukabiliana na msongamano, ikiwemo kupunguza foleni.
Maelekezo ya kupelekwa kwa mizani hiyo ya kupima malori yakiwa kwenye mwenendo yametokana na maombi ya wabunge wa mkoa huo, David Siliinde na Japheti Hasunga ambao kwa pamoja waliomba serikali kupeleka mizani katika eneo hilo ili kukabili tatizo la foleni.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi, Suleiman Bishanga, alisema utekelezaji wa mradi huo, chini ya Mkandarasi wa Kampuni ya Mehrab ya Jijini Mbeya amesema, serikali tayari imetoa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza ambao unaendelea sasa.
Mhandisi Bishanga mesema eneo hilo la maegesho linalotengenezwa sasa litakuwa na uwezo wa kupokea malori kati ya 150 hadi 200 na lengo ni kulifanya eneo hilo kuwa huduma zote muhimu.
Aidha, Mhandisi Bishanga amesema awamu ya pili ya mradi huo utakapokamilika utafanya maegesho hayo kuwa na uwezo wa kuegesha malori 600.









0 Comments